HABARI ZA MICHEZO

Usain Bolt asema kwaheri kwa 'kila kitu' na kustaafu

 Usain Bolt

Usain Bolt amesema alikuwa "anasema kwaheri kwa kila kitu" na alikuwa "karibu kulia" alipokuwa anafikisha kikomo maisha yake kama mwanariadha katika mashindano ya ubingwa wa dunia jijini London.
Bolt, 30, mshindi wa dhahabu mara nane katika Olimpiki, amestaafu kutoka kwenye riadha baada ya kung'aa sana na kujizolea umaarufu si haba.
"Inasikitisha kwamba inanilazimu kuondoka sasa," alisema raia huyo wa Jamaica, ambaye alikimbia kuzunguka uwanja kuwaaga wachezaji uwanja wa michezo wa London Jumapili usiku wa kufungwa kwa mashindano hayo.
"Nilikuwa nasema kwaheri kwa mashabiki na kwaheri kwa mashindano niliyokuwa nashiriki pia."
Alipoulizwa iwapo atarejea kushindana tena, alijibu: "Nimewaona watu wengi sana wakistaafu na kurudi tena halafu hali yao inakuwa mbaya zaidi au wanajiaibisha.
"Sitakuwa mmoja wa watu hao."
Bolt alishinda shaba mbio zake za mwisho za mita 100 kisha akaumia na kushindwa kumaliza mbio za kupokezana vijiti za 4x100m Jumamosi usiku.
Hii ina maana kwamba bingwa huyo wa dunia mara 19, ambaye Lord Coe alimfananisha na Muhammad Ali, aliondoka kwa njia isiyo ya kawaida - akisaidiwa kuondoka uwanjani na wenzake, akiwa hawezi kusimama vyema wima baada ya kuumia.
"Kwangu, sidhani mashindano haya yatabadilisha yote niliyoyafanya,2 aliongeza.
"Nakumbuka baada ya kushindwa mbio za 100m, kuna mtu alinijia na kuniambia, 'Usain, usiwe na wasiwasi, Muhammad Ali alishindwa pigano lake la mwisho, hivyo usisikitike sana kuhusu hilo'.
"Nimedhihirisha ustadi wangu, mwaka baada ya mwaka, katika kipindi changu chote nilichoshiriki mbio hizi. Nilikuwa nasema kwaheri kwa kila kitu. Nilikuwa karibu kulia. Nilikaribia sana, lakini machozi hayakutoka."

 

Diego Costa asema Chelsea wanamchukulia kama 'mhalifu'

 Diego Costa

Diego Costa amesema Chelsea wamekuwa wakimchukulia kama "mhalifu" na akathibitisha kwamba bado anataka kurejea Atletico Madrid.
Mshambuliaji huyo wa miaka 28 alichezea Chelsea mara ya mwisho fainali ya Kombe la FA mwezi Mei na mwezi Juni alitumiwa ujumbe wa simu na meneja Antonio Conte kumfahamisha kwamba hakuwa kwenye mipango yake ya msimu ulioanza siku chache zilizopita.
Costa amesema sasa klabu hiyo inamshurutisha kurejea akafanye mazoezi na wachezaji wa akiba.
"Ni kwa nini hawataki kuniacha niondoke iwapo hawanitaki?" aliambia Daily Mail.
"Lazima nifanye yale inanibidi kuyafanya. Lazima nifikirie kuhsuu maslahi yangu. Nimekuwa mvulana mzuri hapa na nilijaribu kufanya kila kitu sawa. Mapenzi yangu ni kwenda Atletico."
Costa anaamini kwamba meneja Antonio Conte ndiye anayemchongea.
"Januari, mambo yalifanyika kati yangu na kocha. Nilikuwa nimekaribia sana kutia saini mkataba mpya lakini akasimamisha hilo. Nashuku meneja alihusika. Aliomba hilo lifanyike.
"Mawazo yake ni wazi na hayabadiliki. Nimeona yeye ni mtu wa aina gani. Ana mtazamo wake na huo hautabadilika.
"Namheshimu sana kama kocha. Amefanya kazi nzuri na naona hilo, lakini kama binadamu, la. Si mkufunzi ambaye ana uhusiano wa karibu na wachezaji. Hukaa mbali. Hana sifa za kuhusiana vyema na wachezaji.
Juni, Costa alitumiwa arafa na Conte kufahamishwa hangekuwa kwenye mipango ya timu.
"Sijaufuta ujumbe huo wa simu. Watu wakinituhumu kwamba nasema uongo, naweza kuwaonesha. Ujumbe huo ulikuwa wazi, alisema simo kwenye mipango yake na akanitakia kila la kheri siku zijazo. Weka kikomo hapo."
Mshambuliaji huyo wa Uhispania alipewa muda zaidi kupumzika na Chelsea mwezi jana lakini sasa anasema anaadhibiwa kwa hilo.
Anasema anatozwa faini kwa kutokuwa kwenye klabu muda huo na amesema anafikiria kwenda kortini au kujaribu kumaliza sehemu iliyosalia ya mkataba wake bila ujira nchini Brazil.
"Unajua meneja hanitaki," aliongeza Conte.
"Nasubiri Chelsea waniachilie huru. Sitaki kuondoka. Nilikuwa na furaha. meneja asipokutana, ni lazima uondoke."
Costa ambaye ni mzaliwa wa Brazil lakini huchezea timu ya taifa ya Uhispania alijiunga na Chelsea kutoka Atletico Madrid kwa £32m mwaka 2014.
Alikaa misimu minne Atletico na alikuwa amedokeza kwamba huenda akarejea katika klabu hiyo.
Lakini klabu hiyo ya La Liga imepigwa marufuku kununua wachezaji hadi Januari.
"Kukaa miezi mitano bila kucheza? Sijui, ni kizungumkuti, lakini watu wanajua kwamba naipenda sana Atletico na kwamba huwa napenda kukaa Madrid," Costa alisema mwezi Juni.
Januari, Costa aliachwa nje ya kikosi cha Chelsea kilichosafiri kucheza mechi ugenini Leicester baada yake kukorofishana na mkufunzi wa mazoezi.
Hilo lilitokea baada ya kuibuka kwa taarifa kwamba alikuwa amepata ofa kutoka China ya kulipwa mshahara wa £30m kwa mwaka. Wakati huo, Chelsea walisema hawakuwa na nia ya kumuuza.
Baadaye Januari, mmiliki wa Tianjin Quanjian alisema juhudi zao za kutaka kumnunua Costa zilitatizwa na sheria mpya kuhusu wachezaji wa kutoka nje Ligi Kuu ya Uchina.
Kuanzia msimu ujao, klabu za Uchina zinaruhusiwa kuchezesha wachezaji watatu pekee kutoka nje ya nchi kwenye mechi badala ya wanne kama ilivyokuwa awali.

 

TUESDAY 15/08/2017

Ronaldo apigwa marufuku ya mechi tano

Ronaldo baada ya kupewa kadi nyekundu

Mchezaji nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo amepewa marufuku ya mechi tano baada kupewa kadi nyekundi wakati wa mechi ya el Clasicco siku ya Jumapili.
Alipewa marufuku ya mechi moja kwa kuonyeshwa kandi mbili za njano na nyengine nne kwa kumsukuma refa kutoka nyuma baada ya kutolewa nje.
Alipewa kadi nyekundu kwa kuvua tishati yake alipokuwa akisherehekea bao lake lililofanya mambo kuwa 2-1 na kujirusha
Atakosa mechi ya Jumatano ya awamu ya pili.
Ronaldo ana siku 10 kukata rufaa.
Raia huyo wa Ureno atacheza katika ligi ya mabingwa lakini hatocheza hadi tarehe 20 mwezi Septemba dhidi ya Real Betis.
Madrid tayari ilikuwa ishatoa ishara za kutaka kukata rufaa dhidi ya kadi ya pili ya njano dakika nane kabla ya mchezo kukamilika alipojiangusha ndani ya eneo hatari baada ya kubanwa na Samuel Umtiti.

 

MSUVA KWENDA MOROCCO JUMATANO KUKAMILISHA UHAMISHO WAKE DIFAA EL-JADIDA


WINGA wa Yanga SC, Simon Msuva anatarajiwa kuondoka nchini Jumatano kwenda Morocco kwa ajiloi ya kukamilisha uhamisho wake kujiunga na Difaa Hassani El-Jadida ya Ligi Kuu ya nchini humo.
Difaa ambayo tayari imekwishamchukua Mtanzania mwingine, winga pia Ramadhani Singano ‘Messi’ kutoka Azam FC iko tayari kutoa dola 150,000 kumnunua Msuva ambaye amebakiza miezi tisa katika mkataba wake Yanga.
Akizungumza  Msuva amesema kwamba akifuzu vipimo vya afya atasaini moja kwa moja mkataba wa kujiunga na timu hiyo ya Ligi Kuu ya Morroco.

Msuva amerejea Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo kutoka mjini Kigali alipokuwa na kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya mchezo na wenyeji, Rwanda kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN.
Taifa Stars imeondolewa mapema kwenye michuano ya CHAN, inayoshirikisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee, baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 juzi na wenyeji Rwanda Uwanja wa Kigali, uliopo Nyamirambo mjini Kigali, hivyo kuondolewa kwa bao la ugenini, kufuatia kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Jumamosi iliyopita.
“Ninamshukuru Mungu nimerudi salama kutoka Rwanda na Jumatano ninaanza safari ya kuelekea nchini Morocco kumalizia taratibu zilizobakia,”alisema Msuva aliyejiunga na Yanga mwaka 2012 akitokea Moro United.
Timu hiyo yenye maskani yake mji wa El Jadida ikiwa inatumia Uwanja wa El Abdi inataka kuwatumia mawinga wa Tanzania kujaribu kutwaa taji la kwanza la Ligi Kuu ya Morocco, inayojulikana kama Botola, moja ya Ligi bora kabisa barani Afrika.

 

 

ERASTO NYONI AIGEUKA YANGA, ASAINI SIMBA MIAKA MIWILI


KLABU ya Simba imewazidi ujanja mahasimu, Yanga baada ya kufanikiwa kukamilisha usajili wa mchezaji kiraka, Erasto Edward Nyoni kutoka Azam FC kama mchezaji huru.
Nyoni leo amesaini mkataba wa miaka miwili pamoja na kipa Said Mohammed Mduda kabla ya kwenda Rwanda na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Amavubi Jumamosi mjini Kigali kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
Habari za kiungo huyo anayeweza kucheza nafasi zote za ulinzi, Nyoni kwenda Simba ni pigo kwa Yanga, ambao walikuwa wamekwishaanza naye mazungumzo.
Erasto Nyoni leo amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Simba akitokea Azam FC kama mchezaji huru

Erasto ni mchezaji pekee ambaye alikuwepo timu ya taifa kanzia wakati wa Mbrazil, Marcio Maximo mwaka 2006 na ameendelea kuitwa na kila kocha aliyefuatia kupewa jukumu la kuifundisha timu hiyo kuanzia Wadenmark Jan Borge Poulsen, Kim Poulsen, Mholanzi, Mart Nooij na wazalendo Mkwasa na huyu wa sasa, Salum Mayanga.
Pamoja na kucheza nafasi za ulinzi, lakini Nyoni ameifungia Stars mabao manne ya kukumbukwa, likiwemo bao pekee katika ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya wenyeji Burkina Faso, Juni 16, mwaka 2007 mjini Ouagadougou katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2010.
Na hilo ndilo lilikuwa bao lake la kwanza Taifa Sars kabla ya kufunga tena Juni 10, mwaka 2012 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bao la ushindi, Tanzania ikiilaza 2-1 Gambia katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia.
Akafunga bao la kwanza katika sare ya 3-3 na wenyeji Botswana Uwanja wa Molepolole mjini Molepolole, Agosti 15, 2012 kwenye mchezo wa kirafiki, kabla ya Julai 5, mwaka huu kufunga bao la kwanza katika Nusu Fainali ya Kombe la COSAFA Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini Taifa Stars ikifungwa 4-2 na Zambia waliotoka nyuma kwa 1-0.
Nyoni ambaye Mei 7, mwaka huu amefikisha miaka 29, amekuwa mchezaji wa Azam FC tangu mwaka 2010 alipojiunga nayo kutoka Vital’O ya Burundi iliyomchukua AFC ya Arusha alikocheza kidogo tu akitokea kituo cha Rollingston cha mjini humo.

YANGA YAMTIA KITANZI KAMUSOKO MIAKA MIWILI

Thabani Kamusoko

KIUNGO Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko leo amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea Yanga baada ya mavutano na uongozi kwa takriban mwezi mmoja.
Baada ya kusaini mkataba huo mpya utakaomfanya adumu Jangwani hadi Julai 2019, Kamusoko atajiunga na wenzake kwa mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya.
Mchezaji huyo mtaalamu wa kugawa pasi, alisajiliwa Yanga SC mwaka 2015 kutoka FC Platinums ya kwao, Zimbabwe pamoja na mshambuliaji Donald Ngoma, ambaye naye tayari ameongeza mkataba Jangwani. 
Wachezaji 16 tayari wapo mazoezini Yanga SC kwa sasa wakiendelea na maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina.
Hao ni pamoja wapya wanne, kipa Mcameroon, Youthe Rostand aliyesajiliwa kutoka African Lyon, beki Abdallah Hajji ‘Ninja’ kutoka Taifa Jang’ombe, kiungo Pius Buswita kutoka Mbao FC na mshambuliaji Ibrahim Ajib kutoka kwa mahasimu, Simba SC.
Wengine ni mabeki, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Abdul, Pato Ngonyani, Mwinyi Hajji Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, viungo Geoffrey Mwashiuya, Juma Mahadhi, Said Juma Makapu, Emmanuel Martin, Yussuf Mhilu, Obrey Chirwa na mshambuliaji Amissi Tambwe.
Wachezaji ambao hawapo ni pamoja na majeruhi watatu, kipa Benno Kakolanya, kiungo Deus Kaseke na Ngoma ambaye anatarajiwa kurejea wakati wowote kutoka Afrika Kusini alipokwenda kwa matibabu.
Beki Hassan Kessy na winga Simon Msuva wapo na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars ambacho leo kimekwenda Kigali, Rwanda kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Rwanda mwisjoni mwa wiki kuwania tiketi ya CHAN 2018 nchini Kenya, baada ya sare ya 1-1 Jumamosi mjini Mwanza.

 

PANUCCI APEWA KAZI YA KUINOA ALBANIA.

 Panucci

Chama cha soka cha nchini Albania (AfA) kimemteua beki wa zamani wa timu ya taifa ya Italia Christian Panucci kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo.
Panucci anachukua mikoba ya kocha wa zamani wa taifa hilo Gianni De Biasi,ambae alijiuzulu mwezi uliopita.
Raisi wa chama hicho cha soka Armand Duka amesema kazi ya kwanza ya kocha huyo mpya ni kufuzu kwa fainali za michuano ya ulaya ya 2020.
Panucci aliwahi kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Urusi chini ya Fabio Capell, pia amewahi kuvifundisha vilabu vya Livorno na Ternana vya Seria B.na amewahi kuvichezea vilabu vya Real Madrid na As Roma,

 

 AGUERO HAUZWI ASEMA GUARDIOLA

 GUARDIOLA

Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amethibitisha hana mpango wa kuuza mshambuliaji wake Sergio Aguero kun.
"Ni mchezaji wetu na atabakia hapa,"alisema Guardiola wakati akizungumzia tetesi za mchezaji huyo huenda akaondoka.
Hata hivyo kocha huyo amesema wanahitaji kusajili wachezaji wengine watatu au wanne katika kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao.
Man City imekua kwenye mawindo ya kuwania saini za walinzi Danilo wa Real Madrid na Benjamin Mendy anayekipiga na katika timu ya Monaco, pamoja na mshambuliaji hatari wa Arsenal Alexis Sanchez.

 

ANTONIO CONTE: MENEJA WA CHELSEA  ASAINI KANDARASI  MPYA YA MIAKA 2. 

Meneja wa Mabingwa wa England Chelsea, Antonio Conte, amesaini Mkataba Mpya ulioboreshwa wa Miaka Miwili.
Dili hii haiongezi muda wake wa Mkataba wa Miaka Mitatu aliosaini Mwaka 2016 bali imempa maslahi bora zaidi.
 
Meneja huyo kutoka Italy mwenye Miaka 47 amesema amefurahishwa mno na Mkataba huu Mpya na kuahidi kufanya bidii zaidi kupita Mwaka wake wa
kwanza uliozaa Ubingwa wa EPL, LIGI KUU ENGLAND.
Wakielekea kutwaa Ubingwa, Kikosi cha Conte kilishinda Jumla ya Mechi 30 zikiwemo 13 mfululizo ambayo ni Rekodi kwa Chelsea.
Mbali ya Ubingwa huo, Conte pia aliiongoza Chelsea kufika Fainali ya FA CUP waliyofungwa na Arsenal.
Ujio wa Conte huko Stamford, ulimwezesha Kocha huyo wa zamani wa Juventus na Timu ya Taifa ya Italy kuigeuza Chelsea iliyomaliza Nafasi ya 10 kwenye EPL Msimu wa kabla yake na kutwaa Ubingwa kwa kishindo.
Wachambuzi wanahisi mafanikio hayo yaliletwa na uamuzi wa Conte wa kugeuza mtindo wao wa Mazoezi na pia Mfumo wa Uchezaji wa kutumia Mabeki Watatu katika Fomesheni ya 3-4-3.

Chelsea – Mechi kuelekea Msimu Mpya:
22 Julai v Arsenal, Bird’s Nest Stadium, Beijing
25 Julai v Bayern Munich, National Stadium, Singapore (International Champions Cup)
29 Julai v Inter Milan, National Stadium, Singapore (International Champions Cup)
6 Agosti v Arsenal, Wembley Stadium (Community Shield)

 Habari: Michezo

SAMPDORIA YATOA OFA KUMNUNUA JACK WILSHERE!
 WISHERESampdoria ya Italy imetoa Ofa ya Pauni Milioni 6 pamoja na nyongeza kadhaa za Pauni Milioni 1.5 kumnunua Kiungo wa Arsenal Jack Wilshere.

Wilshere amebakiza Mwaka Mmoja kwenye Mkataba wake na Arsenal na Msimu ulopita alikuwa kwa Mkopo huko Bournemouth.
Hata hivyo Mchezaji huyo mwenye Miaka 25 na ambae ameichezea England mara 34 hakumaliza Msimu baada ya kuvunjika Mguu kwenye Mechi na Tottenham Mwezi Aprili.
Pia iliwahi kuripotiwa kuwa Wilshere atapelekwa kwa Mkopo huko Crystal Palace.
Lakini Wikiendi iliyopita Meneja wa Arsenal Arsene Wenger alieleza kuwa anatarajia Wilshere atabaki Arsenal na kupigania namba yake.

 Habari: Michezo

ARSENAL KUTUMIA CHIPUKIZI EUROPA LIGI!


EUROPALIGI NICE 2
ARSENE WENGER ameripotiwa kuwa atawatumia Chipukizi wake kwenye Mashindano ya UEFA EUROPA LIGI ili Kikosi cha Kwanza cha Arsenal kitilie mkazo mbio za Ubingwa za EPL, LIGI KUU ENGLAND.
Wenger, ambae ameongezewa Mkataba wa Miaka Miwili wa kuwa Meneja wa Arsenal, yuko kwenye presha kubwa ya kuhakikisha Klabu hiyo inafanikiwa kwenye Msimu Mpya wa 2017/18. 
Msimu uliopita Arsenal ilimaliza Nafasi ya 5 kwenye EPL na hivyo kukosa kucheza UEFA CHAMPIONZ LIGI kwa mara ya kwanza katika Miaka 20.
Pia Arsenal hawajatwaa Ubingwa wa England tangu 2004.
Kwa mujibu wa duru za ndani ya Arsenal, Wenger hatawatumia Mastaa wake wakubwa kama  vile Alexis Sanchez, Alexandre Lacazette na Mesut Ozil kwenye UEFA EUROPA LIGI ili wakaze kwenye EPL.
Kwenye UEFA EUROPA LIGI Arsenal itaanzia Hatua ya Makundi na Droo ya kupanga Makundi hayo itafanyika Agosti 25.

Habari: Michezo


FEDERER APANDA JUU KATIKA VIWANGO VYA UBORA.

Mshindi wa taji la Wimbedon Roger Federer amepanda kwenye viwango vya ubora wa mchezo huo kutoka nafasi ya tano mpaka nafasi ya tatu
Mwingereza Andy Murray anaendelea kuwa kinara katika nafasi ya kwanza, Rafael Nadali akifuatia katika nafasi ya pili, Novak Djokovic ni namba nne kwa ubora, huku Stan Wawrinka akiwa katika nafasi ya tano.
Kwa upande wa wanawake Karolina Pliskova ndie kinara akifuatiwa na Simona Halep
Mjerumani Angelique Kerber yuko katika nafasi ya tatu na Johanna Konta akishika nafasi ya nne na Garbine Muguruza anakamilisha tano bora.

No comments:

Post a Comment