Bunge la Niger limepiga kura kwa
kauli moja, kutuma vikosi nchini Nigeria kujiunga na mapambano ya kikanda dhidi
ya kundi la Boko Haram. Kulingana na azimio la bunge hilo, Niger itatuma
wanajeshi 750 nchini Nigeria.
Wavuvi hawaendi tena ziwani kuvua, wakulima
hawaendi tena mashambani, shule zimefungwa. Wakaazi wa maeneo ya mpakani ya
Diffa na Bosso, kusini mwa Niger wamejawa na hofu, kutokana na magaidi
waliojigeuza wapiganaji wa jihadi, ambao wanatishia usalama wa taifa lao."
Hao ni makatili tu wasioheshimu sheria, wanaiba, kuuwa, na kubaka,"
alisema Abdou Lokoko, mfanyakazi wa shirika lisilo la kiserikali nchini Niger.
Kwa mara
ya kwanza wapiganaji hao kutoka kaskazini mwa Nigeria wameshambulia maeneo ya
upande wa Niger katika siku chache zilizopita. Siku ya Jumatatu, wakati bunge
likijiandaa na kura hiyo, Boko Haram waliushambulia mji wa Diffa wenye wakaazi
60,000 na kuuwa watu watano.
Jeshi
lilifanikiwa kuwafurusha, kwa mujibu wa maelezo yake, lakini muda mfupi baadae,
ilifuatia miripuko ya mabomu.Katika mashambulizi sawa na hayo wiki iliyopita,
mamia ya wapiganaji wa Boko Haram waliripotiwa kuuawa katika miji ya Diffa na
Bosso, pia wanajeshi kadhaa na raia pia walipoteza maisha.
"Tuna
ushahidi wa Boko Haram kuendesha harakati zake ndani ya Niger, na hiyo ni tangu
mwaka 2012, wakati washukiwa kadhaa wa Boko harama walipokamatwa na maafisa wa
idara ya usalama ya Niger, hasa katika mikoa wa Zinder na Diffa iliyoko mpakani
na Nigeria," alisema Ryan Cummings, mchambuzi wa masuala ya usalama wa
shirika la ushauri la red.24 la Afrika Kusini, ambalo ni sehemu ya mtandao wa
usalama wa Nigeria.
Kikosi cha pamoja dhidi ya Boko Haram
"Yeyote anaetaka amani laazima ajiandae na vita hivi," alisema Abdou Lokoko, ambaye pamoja na shirika lake wamekuwa wakitoa wito wa kujenga kikosi cha pamoja dhidi ya Boko Haram. "Ikiwa hatutofanya chochote, basi wataendelea kutushambulia. Wanajeshi wetu ni mashujaa na wako tayari kwa mapambano. Mungu akipenda watatulinda."
Jeshi kamili la magaidi
Lakini kumuamini Mungu tu hakutowasaidia wanajeshi hao. Taarifa mpya za mashirika ya ujasusi ya Marekani zinaonyesha kuwa Boko Haram ina wapiganaji kati ya 4000 na 6000. Katika maeneo yaliyoko chini ya udhibiti wake, kundi hilo lina mtandao wa miji na vijiji 30, ambako linaweza kuwandikisha wapiganaji.
Idadi hii haimshangazi mtaalamu wa masuala ya usalama Ryan Cummings. Anasema huenda wapiganaji wa Boko Haram ni wengi zaidi kuliko idadi hiyo. "Hao ndiyo wale wapiganaji wa itikadi kali waliofunzwa vizuri. Kuna wapiganaji wa ziada, ambao ama wanaandikishwa kwa nguvu, au wanalipwa.Kuna uvumi pia kuwa kundi hilo linakodi magenge yenye silaha."
Kwa hilo kundi hilo la kigaidi limeunda jeshi kamili tangu muda mrefu. Na pia lina kiongozi anaependa kujionyesha kwa jamii kama mtu asiye na mzaha.Katika mkanda wake wa video wa karibuni, Abubakar Shekau anaonekana akiapa kukishinda vibaya kikosi hicho cha kanda.
"Tutamkamata mmoja baada ya mweingine," alitishia Shekau, akiyalenga mataifa yanayoshiriki operesheni dhidi ya kundi lake. Lakini Mchambuzi Ryan Cummings anaamini jeshi la pamoja litaweza kuidhofisha Boko Haram.
"Kundi hilo litalaazimika kwa mara ya kwanza kupambana kwenye nyanja tofauti kwa wakati mmoja. Hadi sasa Boko Haram ilikuwa inapambana na jeshi la Nigeria kutokea upande wa magharibi. Kwa nchi za Chad, Cameroon, Benin na Niger kujiunga na mapambano hayo, kundi hilo sasa litakabiliwa kwenye maeneo ya mashariki na kaskazini.
Changamoto zinazowakabili washirika
Lakini hilo linahitaji rasilimali: Wanajeshi, silaha, na vifaa vingine. Hilo litalipa kundi hilo changamoto kubwa na linaweza kudhoofisha kwa kiasi kikubwa, anasema Cummings. Lakini kikosi hicho cha kimataifa kinakabiliwa na changamoto kubwa sana. Ukosefu wa kuaminiana kati ya mataifa washirika, mizozo inayotokana na eneo lenye utajiri wa rasilimali kwenye ziwa Chad, ni vikwazo tosha.
Lakini suala la ufadhili haliko bayana. Umoja wa Mataifa ulitaka kushiriki kwa kuwezesha usafiri, Umoja wa Afrika ulikuwa bado haufikia uamuzi wowote.