Saturday, October 13, 2018

Waziri Mkuu Aitisha Nyaraka Za Uendeshaji Soko La Kibaigwa.....Ni baada ya wafanyabiashara na mbunge kulalamikia uendeshwaji wake

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wasimamizi na waendeshaji wa Soko la Kimataifa la Mazao Mchanganyiko la Kibaigwa pamoja viongozi wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kufika ofisini kwake Oktoba 22, 2018 wakiwa na nyaraka zote zinazoonesha uendeshaji wa soko hilo.

Pia Waziri Mkuu ameitaka Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Seleman Jafo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa uendeshaji wa soko hilo kufika na ripoti ya uchunguzi uliofanywa kuhushu uendeshaji wa soko la Kibaigwa siku hiyo.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo Alhamisi, Oktoba 11, 2018 wakati alipohutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi ya Kibaigwa uliopo kwenye Mji Mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa, Dodoma.

“Nawataka ofisini kwangu, bodi ya uendeshaji wa soko, menejimenti nzima pamoja na tume iliyoundwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI na viongozi wa MVIWATA, mkiwa na nyaraka zote za uendeshaji soko hili.”

Waziri Mkuu alisema baada ya kukutana na viongozi wanaoendesha soko hilo siku ya Jumatatu, Oktoba 22, mwaka huu, saa 2.00 asubuhi, pia atatuma wakaguzi wa ndani kwenda kufanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za soko hilo.

Alisema kumekuwa na mambo yasiyoridhisha kuhusu uendeshaji wa soko la Kibaigwa, hivyo mara baada ya kukutana na menejimenti, bodi, MVIWATA na kupata nyaraka za uendeshaji, atatuma wataalamu kwenda kukagua mahesabu yake ili kubaini kinachoendelea.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na wafanyabishara wakidai soko hilo limekuwa na matatizo mengi yakiwemo ya uchakavu na mapato yake kutowanufaisha wananchi.

Walisema pamoja na matatizo ya kiutendaji, pia mapato yanayopatikana katika soko hilo hayainufaishi Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kibaigwa, hivyo viongozi wake wanashindwa kuboresha miundombinu yake pamoja na kuliendeleza.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Job Ndugai alisema uendeshaji wa soko hilo umehodhiwa na MVIWATA hivyo kulifanya Baraza la Madiwani la Mji Mdogo wa Kibaigwa kutokuwa na sauti ya kuamua mambo yake.

Ndugai ambaye ni Spika wa Bunge, alisema MVIWATA walitakiwa kuwa washauri tu badala ya kuwa ndio wasemaji wakuu wa uendeshaji wa soko hilo la mazao mchanganyiko la kimataifa la Kibwaigwa, kwa sababu jukumu hilo ni la madiwani.

No comments:

Post a Comment