Tuesday, August 15, 2017

USAIN BOLT ASEMA KWAHERI KWA 'KILA KITU' NA KUSTAAFU.



Usain Bolt amesema alikuwa "anasema kwaheri kwa kila kitu" na alikuwa "karibu kulia" alipokuwa anafikisha kikomo maisha yake kama mwanariadha katika mashindano ya ubingwa wa dunia jijini London.
Bolt, 30, mshindi wa dhahabu mara nane katika Olimpiki, amestaafu kutoka kwenye riadha baada ya kung'aa sana na kujizolea umaarufu si haba.
"Inasikitisha kwamba inanilazimu kuondoka sasa," alisema raia huyo wa Jamaica, ambaye alikimbia kuzunguka uwanja kuwaaga wachezaji uwanja wa michezo wa London Jumapili usiku wa kufungwa kwa mashindano hayo.
Usain Bolt
"Nilikuwa nasema kwaheri kwa mashabiki na kwaheri kwa mashindano
niliyokuwa nashiriki pia."
Alipoulizwa iwapo atarejea kushindana tena, alijibu: "Nimewaona watu wengi sana wakistaafu na kurudi tena halafu hali yao inakuwa mbaya zaidi au wanajiaibisha.
"Sitakuwa mmoja wa watu hao."
Bolt alishinda shaba mbio zake za mwisho za mita 100 kisha akaumia na kushindwa kumaliza mbio za kupokezana vijiti za 4x100m Jumamosi usiku.
Hii ina maana kwamba bingwa huyo wa dunia mara 19, ambaye Lord Coe alimfananisha na Muhammad Ali, aliondoka kwa njia isiyo ya kawaida - akisaidiwa kuondoka uwanjani na wenzake, akiwa hawezi kusimama vyema wima baada ya kuumia.
"Kwangu, sidhani mashindano haya yatabadilisha yote niliyoyafanya,2 aliongeza.
"Nakumbuka baada ya kushindwa mbio za 100m, kuna mtu alinijia na kuniambia, 'Usain, usiwe na wasiwasi, Muhammad Ali alishindwa pigano lake la mwisho, hivyo usisikitike sana kuhusu hilo'.
"Nimedhihirisha ustadi wangu, mwaka baada ya mwaka, katika kipindi changu chote nilichoshiriki mbio hizi. Nilikuwa nasema kwaheri kwa kila kitu. Nilikuwa karibu kulia. Nilikaribia sana, lakini machozi hayakutoka."

No comments:

Post a Comment