Kinara wa muungano
upinzani nchini Kenya Raila Odinga, amewashauri wafuasi wake kususia
kazi siku ya Jumatatu kama njia ya kupinga matokeo ya uchaguzi
uliofanyikia Jumanne iliyopita.
Akihutubia wafuasi wake mtaani Kibera, Nairobi kwa mara ya kwanza kabisa tangu kutangazwa matokeo, ambapo Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi, Bw Odinga amedai kuwa serikali ilikiwa imepanga kuwaua wafuasi wa upinzani kabla ya kutangazwa matokeo.
Hii ni siku moja baada wa watu kadha kuripotiwa kuuliwa maeneo tofauti ya mji wa Nairobi na Kisumu, wakati wafuasi wa upinzani walijitokeza kulalamikia matokeo ya uchaguzi
Rais Uhuru Kenyatta alitangzwa mashindi kwa kura 8,203,290 huku naye Raia Odinga akipata kura 6,762,224.
Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, ambaye alikuwa mpatanishi mkuu baada ya mzozo wa kisiasa nchini Kenya miaka kumi iliyopita, alikuwa ametoa wito kwa Bw Odinga kutumia mifumo ya kisheria kutafuta haki kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais.
"Namshukuru kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kampeni ya uchaguzi ya amani aliyoiendesha. Amekuwa mtetezi jasiri wa demokrasia," amesema Dkt Annan kupitia taarifa.
"Kwa hivyo, namhimiza sasa afuatilie malalamiko yake kupitia mifumo ya kisheria iliyowekwa na aweke maslahi ya taifa mbele, kama alivyofanya kwa uzalendo mara nyingi awali."
Mwaka 2007, watu zaidi ya 1,000 walifariki na wengine 600,000 wakafurushwa makwao wakati wa ghasia za kikabila zilizozuka baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
No comments:
Post a Comment