Monday, April 9, 2018

CCM Mwanza yatangaza maandamano Aprili 26


Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza, wanakusudia kufanya maandamano ya amani Aprili 26, mwaka huu, kuunga mkono na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt John Pombe Magufuli

Maandamano hayo yanakuja ikiwa ni jitihada za kuzima kile walichokiita uhuni unaofanywa na wapinzani wao kisiasa wa kutaka kuharibu amani kwa kuhamasisha maandamano ya kuchochea vurugu siku hiyo kupitia mitandao ya kijamii.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Katibu wa chama hicho Mkoa wa Mwanza, Paschal Mwangwala wakati wa kikao maalumu cha uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa kazi za Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Angelina Mabula kwa miaka miwili uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Kiruma, jijini Mwanza na kuhudhuriwa na wajumbe 608 kati ya 748 kutoka kata 19 za jimbo hilo.

Mangwala alisema wana-CCM hawawezi kukaa kimya na kushangilia vitendo vinavyofanywa na wapinzani vya kutaka kuvunja amani, bali wazuie kwa kuandaa maandamano hayo yatakayoeleza kuwa chama pekee nchini ni CCM.

“Saidieni watu waone chama ni CCM peke yake na si vingine vinavyodandia ajenda ya kupiga kelele hiyo Aprili 26, na sisi tusaidiane maandamano ya kumpongeza Rais Magufuli. Haiwezekani watu waongee vitu vya kipuuzi na kukaa kimya.”

“CCM Mwanza hatuwezi kuvumilia yeyote atakayevunja amani, yeyote atakayeleta chokochoko kwenye mkoa wetu atakiona cha mtema kuni. Yanayofanywa na viongozi wetu wa juu yashuke mpaka kule chini, wananchi waone, viongozi wa mitaa waunge juhudi hizi,” alisema.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilemela, Nelson Mesha alisema kinachofanywa na vyama vya upinzani nchini ni dalili tosha kuwa vimefikia mwisho na vimekosa hoja na badala yake vinakimbilia kufanya maandamano.

No comments:

Post a Comment