Tuesday, April 10, 2018

Marekani yaapa kuichukulia hatua Syria

 Rais Donald Trump amesema Marekani inapanga kutoa jibu la nguvu kuhusiana na shambulio la kemikali katika mji wa Douma nchini Syria.

Rais Trump ambaye amekutana na washauri wake wa kijeshi amesema uamuzi unaweza kuchukuliwa katika saa zijazo.

Kauli yake hiyo inafuatia kauli mbalimbali za kulaani shambulio hilo ziliotolewa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Wakati wa kikao hicho, Urusi na Marekani zilijikuta zikitupiana vikali maneno.

Balozi wa Marekani katika baraza hio Nikki Haley amemtuhumu Rais wa Syria Bashar al Assad kwa jinsi alivyowajibika kwa shambulio hilo.

Ametaka kupigwa kura hii leo, juu ya azimio la awali kuweza kufanya uchunguzi mpya juu ya matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria.

Tayari Urusi ambaye ndiye mshirika wa Syria imesema haita unga mkono pendekezo hilo.

Mwakilishi wa Urusi, Vassily Nebenzia amesema tukio lililotokea katika mji wa Douma ni la kupangwa, na kwamba hatua za kijeshi zinazotaka kuchukuliwa na Marekani zinaweza kuwa na athari mbaya.

Akitoa kauli ya nchi yake, Rais Trump amesema tukio hilo litakutana uamuzi aliouita wa nguvu na kuongeza kuwa nchi yake ina njia na maamuzi mengi ya kijeshi na kwamba hatua zitachukulkiwa katika kipindi kifupi.

Naye Mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Jaafari amesema Marekani na washirika wake wamekuwa wakifadhili ugaidi nchini Syria, na ndio wao wanapaswa kuwajibika na shambulio hilo la kemikali.

Kufuatia kikao hicho cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kauli iliyotolewa na Rais Donald Trump, kumekuwa na dalili zinazoonesha kuwa mataifa ya magharibi yataungana na Marekani kupanga hatua za kuchukua.

No comments:

Post a Comment