Rais
 John Magufuli amefichua siri ya kumteua Profesa Ibrahim Juma kuwa Kaimu
 Jaji Mkuu akisema hakuwa na historia ya kutosha ya majaji wengi 
alipoingia madarakani.
Amesema
 alipoingia madaraka ilikuwa kipindi kifupi ambacho aliyekuwa Jaji Mkuu,
 Mohamed Chande Othman alistaafu hivyo ilimlazimu achukue muda mrefu wa 
kujiridhisha na alitumia Ibara ya 118 (4) kumteua Kaimu Jaji Mkuu.
Rais
 Magufuli amesema hayo leo Jumatatu, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati 
wa kumwapisha Jaji Mkuu, Profesa Juma baada ya kumteua jana Jumapili.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
“Nilifanya
 hivi si kwa sababu hakuna majaji au walikuwa hawafai, majaji wote ni 
wazuri na mnafanya kazi nzuri sana lakini sikutaka kuteua jaji baada ya 
mwaka mmoja nateua tena au baada ya miaka miwili anastaafu, nilitaka 
nikiteua akae miaka hata 10, awe ‘anatujaji’ wote tutakaokuwepo,” 
amesema Rais Magufuli.
Amesema
 kumteua Jaji Mkuu ni kazi ngumu, lazima ujue historia na tabia zake, 
pia kuangalia iwapo ataweza kuendana na dhamira yake ya kupambana na 
rushwa.
Rais
 Magufuli amesema rushwa ipo kila sehemu, hivyo baada ya kuchaguliwa na 
wananchi mwaka 2015 alikaa chini na kumwomba Mungu apate kiongozi 
atakayeenda kulisimamia jambo hilo kwa kipindi kirefu zaidi.
Amesema wapo majaji wengi na wenye sifa lakini baadhi yao wamebakisha muda mchache kustaafu.
“Katika
 kufanya uchambuzi wangu nikamwona Profesa Juma ambaye alikidhi vigezo 
vyangu. Nakupongeza sana Profesa Juma ni Mungu ambaye amekuchagua kwa 
hiyo, kawatumikie vizuri watu wa Mungu na utangulize mbele masilahi ya 
Watanzania,” amesema.
Rais
 Magufuli amesema ingawa bado kuna changamoto mbalimbali katika Mhimili 
huo, alimuhakikishia Profesa Juma kwamba Serikali inazitambua na 
aliwataka majaji kutembea kifua mbele kwa kuwa Serikali inatambua kazi 
nzuri wanayoifanya.
Amesema kazi nzuri yoyote haikosi watu wa kuiponda, akitumia msemo wa mti wenye matunda ndiyo unaopopolewa kwa mawe.
Kiongozi
 huyo mkuu wa nchi amesema alipomteua kuwa Kaimu Jaji alipondwa lakini 
alikuwa mvumilivu na hakupata shinikizo la mtu yeyote la kumteua Jaji 
Mkuu.
 

 
No comments:
Post a Comment