Saturday, June 9, 2018

KARIA AWAPA YANGA SAA 48 KUTENGUA KAULI YA KUJITOA KOMBE LA KAGAME, VINGINEVYO…



RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ameutaka uongozi wa klabu ya Yanga kutoa jibu linaloeleweka hadi kufika Jumapili juu ya kujitoa kwao kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Kauli hiyo ya Karia leo, inafuatia Yanga kuiandikia barua TFF kuwaarifu kutoshiriki michuano hiyo kutokana na kubanwa na ratiba ya mashindano mengine.

Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Rais Karia amesema kwamba sababu walizozitoa Yanga hazina mashiko, kwani hata timu nyingine zinazoshiriki michuano hiyo nazo zina ratiba ngumu pia.
“Sababu walizozitoa Yanga juu ya kutoshiriki michuano ya Kagame hazina mashiko, maana si Yanga peke yao ambao ratiba imewabana na ukiangalia hiyo michuano ya Shirikisho Afrika hata Gor Mahia pia wapo, mashindano ya Sportspesa Super Cup ambayo mpaka hivi sasa Gor Mahia wapo na wanacheza fainali Jumapili na Simba,” amesema Karia na kuongeza; “Hivyo kabla hata hatujalipeleka suala hili CECAFA, nauomba uongozi wa Yanga hadi kufika jumapili uwe umetoa jibu la kueleweka juu ya mashindano hayo,”amesema Karia.

Yanga SC imeandika barua TFF leo ikiiarifu kujitoa kwenye Kombe la Kagame ikiwa ni siku tatu tu tangu kutajwa kwa ratiba, ikipangwa Kundi A na mahasimu wao, Simba SC. 
Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam, Afisa Habari wa Yanga, Dissmas Ten amesema kwamba wamepeleka barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kujitoa kutokana na kubanwa na ratiba ya mashindano.
“Ni kweli hatutashiriki mashindano ya Kagame Cup kutokana na ratiba kuwa ngumu kwa upande wetu, kumekuwa na msongamano wa mashindano baada ya kumalizika kwa ligi tumeenda Kenya kwenye michuano ya SportSpesa Super Cup, tumerudi majuzi tu hapa,”
“Pia tuna mechi nyingine ya Kombe la Shirikisho Afrika tutakayocheza nchini Kenya Juni 16 mwaka huu dhidi ya Gor Mahia, hivyo ukiangalia msongamano huo hata wachezaji wetu watakosa muda wa kupumzika, hivyo tumeona ni bora kutoshiriki mashindano hayo ili kuwapa muda wachezaji wetu ili waweze kujiandaa na mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika,”amesema Ten.
Juni 5, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limetaja ratifa ya Kombe la Kagame, michuano inayotarajiwa kuanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu mjini Dar es Salaam na vigogo wa soka Tanzania, Simba SC na Yanga SC watamenyana Julai 5, mwaka huu katika mechi ya Kundi C.
Akitaja makundi ya michuano hiyo, Katibu wa kudumu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye alisema kwamba pamoja na Simba na Yanga, timu nyingine katika Kundi hilo ni Dakadaha ya Somalia na Saint George ya Ethiopia.
Musonye alisema kwamba Kundi A linaundwa na timu za Azam FC, KCCA ya Uganda, JKU ya Zanzibar na Kator FC wa Sudan Kusini, wakati Kundi B linaundwa na timu za Rayon Sport ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Lydia Ludic ya Burundi na Ports ya Djibouti.
FIFA imeridhia Kagame kufanyika mwezi huu tofauti na agizo lake la kutotaka katika mwezi wa Fainali za Kombe la Dunia yasifanyike mashindano mengine yoyote, kwa sababu washiriki watano wa michuano hiyo wapo kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Afrika, ambayo kwa sasa imesimama kupisha Kombe la Dunia itarejea Julai baada ya kumalizika kwa michuano hiyo nchini Urusi.
Hao ni KCCA ya Uganda iliyopo Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine nne kwenye Kombe la Shirikisho ambazo ni Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sports ya Rwanda, Yanga ya Tanzania zilizopoi Kundi D zote na Al-Hilal ya Sudan iliyopo Kundi A.
Na kwa sababu hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Afrika itakwenda hadi Agosti, mwezi ambao msimu mpya wa Ligi Kuu nyingi duniani huanza – michuano ya Kagame isipofanyika mwezi huu kuna hatari isifanyike tena na mwaka huu kwa mara ya tatu mfululizo.
Azam FC ndiyo mabingwa wa mwisho wa michuano hiyo ilipofanyika Tanzania, walipowafunga Gor Mahia 2-0 katika fainali Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabao ya waliokuwa washambuliaji wake hatari, John Raphael Bocco dakika ya 17 na Muivory Coast, Kipre Herman Tchetche dakika ya 64.
Na hiyo ndiyo ilikuwa michuano iliyomtoa mshambuliaji Mkenya, Michael Olunga ambaye kwa sasa anachezea Girona FC ya Hispania kwa mkopo kutoka Guizhou Zhicheng ya China.
Baada ya kufungha mabao matano akiwa na Gor Mahia na kuibuka mfungaji bora akiwapiku , Osman Bilal Salaheldin wa Al-Khartoum ya Sudan aliyefunga mabao manne sawa na Tchetche wa Azam FC, Olunga akachukuliwa na Djurgardens IF ya Sweden mwaka 2016 iliyomuuza Guizhou Zhicheng mwaka 2017.

No comments:

Post a Comment