Thursday, June 7, 2018

Waziri Mkuu Asisitiza Kuzichukulia Hatua Asasi Za Kiraia


Mbunge wa Longido (CCM) Dkt. Steven Kiruswa ameitaka Serikali kuyafutia usajili Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) ambayo huongeza uchochezi nchini kwa kujishughulisha katika masuala ya siasa na hivyo kuhatarisha amani ya watanzania

Mbunge Dkt. kiruswa amesema hayo leo Juni 7, 2018 Bungeni Jijini Dodoma, wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu, na kuongeza kuwa Mashirika hayo yamekuwa yakifanya shughuli ambazo haziendani na malengo ya kuanzishwa kwake na kutaka kauli ya Serikali kusema ni lini itazifuta Taasisi hizo.

Akijibu swali hilo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema kwamba zipo sheria ambazo zinayaongoza Mashirika hayo baada kupewa usajili na endapo kutatokea ukiukwaji wa Kanuni na taratibu serikali haitasita kuchukua hatua

“Pale ambapo itaibanikia NGO’s hizi hazitimizi wajibu wake na zinafanya shughuli nyingine na zinazopelekea mtafaruku ndani ya jamii, upo utaratibu wa kisheria ambao unachukuliwa kama ambavyo sheria inaruhusu, kwahiyo Serikali itaendelea na utaratibu wake wa kawaida wa kuzipitia hizo NGO’s kuona kazi zinazofanywa ndizo zilizokusudiwa wakati wa usajili”, amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa Mashirika hayo yasiyo ya kiserikali yana umuhimu wake katika nchi, kwasababu husaidia serikali kutimiza baadhi ya majukumu ya kijami kwakuwa serikali haiwezi kufanya kila kitu.
 
by rich voice

No comments:

Post a Comment