Na. Eliphace Marwa – Maelezo
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) leo imetoa taarifa ya mfumuko wa bei kwa
mwezi Mei mwaka huu ambao umepungua hadi kufikia asilimia 3.6
ikilinganishwa na asilimia 3.8 ilivyokuwa kwa mwezi Aprili mwaka huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii
kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo amesema kuwa
kupungua kwa bei kumechangiwa sana na kupungua kwa mfumuko wa bei za
bidhaa za vyakula.
“
Baadhi ya bidhaa za chakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei
ni pamoja na mahindi kwa asilimia 10.3, unga wa mahindi kwa asilimia
12.5, mtama kwa asilimia 13.8, unga wa mihogo kwa asilimia 15.2, viazi
mviringo kwa asilimia 9.0 na mihogo mibichi kwa asilimia 12.6, alisema
bwana Kwesigabo.
Aidha
ameongeza kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka
ulioishia mwezi Mei, 2018 imepungua ikilinganishwa na kasi ilivyokuwa
kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili 2018.
Hali
ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka
ulioishia mwezi Mei, 2018 nchini Uganda umepungua hadi asilimia 1.7
kutoka asilimia 1.8 kwa mwaka ulioishia mwezi aprili 2018.
Aidha
kwa upande wa Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2018
umeongezeka kidogo hadi asilimia 3.95 kutoka asilimia 3.73 kwa mwaka
ulioishia mwezi Aprili, 2018.
Mfumuko wa bei unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.
No comments:
Post a Comment