WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi wawachukulie hatua kali wananchi wote
wanaotumia vibaya namba za mawasiliano za jeshi hilo kwa kutoa taarifa
za uongo kuhusu matukio ya majanga ya moto.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini
kuendelea kutoa mafunzo kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na
kupambana na majanga ya moto pindi yanapotokea katika maeneo yao.
Pia
ameziagiza Halmashauri zote nchini kuwa na magari ya zimamoto pamoja na
magari ya kubeba wagonjwa kwenye vituo vyote vya Zimamoto na Uokoaji
katika maeneo yao.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana (Ijumaa, Juni 8, 2018) wakati alipofanya
ziara katika Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura ya Maafa
pamoja na Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha mkoa wa Ilala.
Amesema
ili kudhibiti wananchi wanaopiga simu za kuomba msaada wa kutaka
kuokolewa, huku kukiwa hakuna tukio lolote la janga la moto lililotokea
kwenye maeneo yao, ni vema watu hao wachukuliwe hatua kali ili iwe
fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo baada ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto
na Uokoaji, Thobias Andengenye kumweleza baadhi ya changamoto
zinazolikabili jeshi hilo kuwa ni pamoja na wananchi kupiga simu wakidai
kuna ajali ya moto imetokea katika maeneo yao na baada watu wa uokoaji
kufika wanabaini ni uongo.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu aziagiza Halmashauri zote nchini kuwa na magari ya
zimamoto pamoja na ya kubebea wagonjwa kwa ajili ya kutoa huduma pindi
majanga yanapotokea kwenye maeneo yao ili kuharakisha utoaji wa huduma
za dharura.
Pia
amelitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuendelea kutoa elimu kwa
wananchi ili kila Mtanzania aweze kuwa na uelewa wa kutoa huduma za
awali pindi majanga ya moto yanapotokea katika maeneo yao ikiwa ni
pamoja na kutumia vifaa vya kuzima moto.
Waziri
Mkuu ambaye alitembelea kituo cha Jeshi la Zimamoto cha Ilala amejionea
magari ya kuzimia moto likiwemo la aina ya Bronto Sky Lift lenye uwezo
wa kufika futi 54 na kuzunguka nyuzi 360.
Alielezwa
kuwa katika Bara la Afrika, magari ya aina hiyo yapo matatu tu, ambayo
yapo nchini Tanzania, Misri na Afrika Kusini. Kwa upande wa Tanzania,
gari hilo lilinunuliwa miaka 10 iliyopita kwa sh. bilioni 1.5.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu alitembelea Kituo cha Operesheni na
Mawasiliano ya Dharura ya Maafa, ambapo aliwasisitiza viongozi wa kituo
hicho kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara yatokanayo na kuishi
kwenye maeneo hatarishi hususan mabondeni.
Waziri
Mkuu alisema licha ya kuwapa elimu, pia wanatakiwa kuwashawishi wakazi
wa maeneo hayo kuondoka kabla ya kutokea kwa maafa badala ya kusubiri
majanga yatokee. Pia aliwataka wawe na mpango wa kuonesha eneo lenye
maafa na kuujulisha umma.
Pia
aliwataka watendaji wanaohusika na kamati za maafa waimarishe
mawasiliano katika ngazi zote kuanzia ya kijiji hadi Taifa na wafanye
kazi kwa ushirikiano ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi pindi
maafa yanapotokea.
Awali,
Waziri Mkuualitembelea Ofisi za Mpiga Chapa wa Serikali jijini Dar es
salaam ambapo mbali na mambo mengine alijionea moja kati ya mitambo ya
kwanza ya Mpiga Chapa wa Serikali uitwao Original Heidelberg wenye
zaidi ya miaka 100 ambao bado unafanya kazi vizuri.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment