Bunge
la Tanzania linatarajia kuwa mwenyeji wa vikao vya Kamati ya Uongozi na
ya Bajeti za Chama cha Wabunge wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Madola–Kanda ya Afrika (CPA-AFRICA REGION) vitakavyofanyika tarehe 9
hadi 14, Julai, 2019 katika Ofisi Ndogo za Bunge la Tanzania, Jijini Dar
es Salaam.
Kamati
hizo zitakutanisha Wajumbe kutoka Mabunge zaidi ya Kumi (10) ya nchi za
Afrika ambapo mbali na Wajumbe hao vikao hivyo pia vinatarajiwa
kuhudhuriwa na Spika wa Bunge la Kenya Mhe. Justin Muturi, Spika wa
Bunge la Sierra Leone Mhe. Dkt. Abbas Bundu, Spika wa Bunge la Uganda
Mhe. Rebbeca Kadaga na Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Job Y. Ndugai
ambaye ndiye mwenyeji wao.
Aidha,
mbali na Maspika hao, vikao hivyo vitahudhuriwa na Naibu Spika wa Bunge
la Cameroon Mhe. Emilia Lifaka, Naibu Spika wa Bunge la Namibia, Mhe.
Bernard Sibalatani na pia Mnadhimu Mkuu wa Bunge la Ghana Mhe. Dkt. Osei
Mensah Bonsu.
Mbali
na vikao vya Kamati, kutakuwa pia na kikao cha Bodi ya Chama cha
Wabunge wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola-Kanda ya Afrika ambacho
kitafanyika tarehe 11 Julai, 2019.
Spika
wa Bunge la Tanzania Mhe. Job Y. Ndugai anatarajiwa kuhudhuria na
kuongoza kikao cha Bodi ya Chama cha Wabunge wa Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Madola–Kanda ya Afrika na pia kutoa hotuba ya ufunguzi wa
kikao cha Kamati ya Uongozi wa chama hicho.
Wajumbe
wengine ambao ni Waheshimiwa Wabunge wanaotarajiwa kuhudhuria katika
vikao hivyo wanatoka katika Mabunge ya nchi za Malawi, Kenya, Nigeria,
Ghana, Sierra Leone, Afrika kusini, Uganda, Namibia, Zambia, Lesotho,
Mauritius na wenyeji Tanzania. Kwa hivi sasa Bunge la Tanzania ndiyo
Sekretarieti ya Chama Chama cha Wabunge wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Madola–Kanda ya Afrika.
Imetolewa na;
KATIBU WA CPA-KANDA YA AFRIKA
8 Julai, 2019
No comments:
Post a Comment