Tuesday, July 9, 2019

Simanzi: Sala ya kuaga miili ya wafanyakazi watano wa Azam Tv yafanyika

Marehemu wafanyakazi wa Azam Tv wamepewa heshima za mwisho


Vilio na simanzi vimetawala katika ofisi za makao makuu ya kampuni ya Azam TV hii leo ambapo wafanyakazi watano wa kampuni hiyo wanaagwa baada ya kufariki kwenye ajali ya barabarani.
Ajali iliyogharimu maisha ya wafanyakazi hao ilitokea Shelui mkoani Singida asubuhi ya Jumatatu Juni 8.

Gari aina ya Coaster iliyowabeba wafanyakazi hao iligongana uso kwa uso na lori. Watu wengine wawili ambao si wafanyakazi wa Azam Media walifikwa na umauti pia.
Wafanyakazi wa Azam TV waliofariki kwenye ajali hiyo ni Salim Mhando (muongozaji wa matangazo), Florence Ndibalema (Mhandisi wa Sauti), Sylvanus Kasongo (Mhandisi Mitambo) na wapiga picha wawili Said Haji na Charles Wandwi.
Miili ya wafanyakazi wa Azam ikiwa imewasiliWafanyakazi watatu wa Azam TV wamejeruhiwa ambao ni Artus Masawe, Mohammed Mwinshehe na Mohammed Mainde.
Miili ya marehemu hao ilifikishwa kwenye viwanja vya Azam Media mishale ya saa sita mchana ikitokea hospitali ya Muhimbili ambapo ilihifadhiwa toka iliporejeshwa kutoka Singida jana usiku.
Ilikuwa ni wakati mgumu kwa wafanyakazi wenzao pamoja na familia za marehemu kuwaaga wafanyakazi hao ambao kifo kiliwakuta wakiwa njiani kuelekea kwenye majukumu yao ya kikazi.
Wanafamilia wa marehemu
Safari yao ilianzia Dar es Salaam na ilikuwa iishie Chato mkoani Geita. Walikuwa wakitarajiwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya uzinduzi wa Hifadhi Mpya ya Taifa ya Burigi Chato.
Watu mbali mbali wakiongozwa na rais wa Tanzania John Magufuli wamekuwa wakituma salamu za rambirambi toka jana.

Viongozi mbalimbali wa taifa na kisiasa wamehudhuria shughuli ya kutoa heshima za mwisho.
Waziri wa Habari wa Tanzania Dkt Harrison Mwakyembe amewaongoza waombolezaji hao.
Viongozi wa kisiasa waliohudhuria ni pamoja na Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa chama cha upinzani Chadema), Zitto Kabwe (Kiongozi chama cha upinzani ACT-Wazalendo), Profesa Ibrahim Lipumba (Mwenyekiti chama cha upinzani CUF) na Humphrey Polepole (Katibu Itikadi na Uenezi chama tawala CCM).
 Waombolezaji
Akiongea kwa niaba ya vyama vya upinzani, Freeman Mbowe ametuma salamu za rambirambi kwa Azam Media na wanahabari wote.
Lakini pia amezitaka mamlaka zote zinazosimamia vyombo vya habari kuhakikisha vyombo hivyo vinafanya shughuli zake kwa uhuru bila kupendelea au kukandamiza upande wowote.
Waziri Mwakyembe naye ametoa salamu za rambirambi kwa niaba ya serikali na kutoa onyo kali juu ya wale wanaochapisha mitandaoni picha za marehemu au majeruhi wa ajali.
"Hili ni onyo la mwisho, hatutaongea tena. Tutatekeleza sheria na kuwafunga, haiwezekani ukakosa utu kwa kutumia simu yako kupiga picha wahanga wa ajali bila kuzingatia utu wao na familia zao."

No comments:

Post a Comment