KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Ajibu Migomba amesaini mkataba wa miaka miwili kurejea klabu yake ya zamani, Simba SC kutoka kwa mahasimu, Yanga SC.
Taarifa ya Simba SC leo mchana imesema kwamba Ajibu ameamua kufanya maamuzi sahihi ya kurudi nyumbani Msimbazi baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.
“Safari ya mtoto kuishi mbali na nyumbani imefikia ukingoni. Ibrahim Ajibu ameamua kufanya maamuzi sahihi ya kurudi nyumbani Msimbazi, ndio amerudi na amesaini mkataba wa miaka miwili kucheza na kuwapa furaha Wanasimba. Karibu nyumbani Ajibu,”imesema taarifa ya Simba.
Ajibu anakuwa mchezaji mpya wa nane kusajiliwa Simba SC na wa tatu mzawa baada ya kipa Beno Kakolanya kutoka Yanga SC ya Dar es Salaam na beki Kennedy Wilson Juma kutoka Singida United ya Singida.
Pamoja na kusaini wachezaji wapya, SImba SC pia imewapa mikataba mipya wachezaji wake kadhaa wa msimu uliopita, wakiwemo kipa Aishi Manula, mabeki Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Nahodha Msaidizi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala, Muivory Coast, Serge Wawa Pascal viungo Jonas Mkude, Mzambia Clatous Chama na washambuliaji Nahodha Mkuu, John Bocco na Meddie Kagere raia wa Rwanda.
No comments:
Post a Comment