Wednesday, November 29, 2017

IGP Sirro Asema mtandao Wa Kiuhalifu Kibiti Umesambaratishwa Kwa Kiasi Kikubwa....Ataka Watoto 13000 Wapatikane Haraka

MKUU wa jeshi la polisi nchini (IGP)Simon Sirro amewahakikishia wananchi mkoani Pwani kuwa silaha zote zilizochukuliwa na wahalifu wa ovyo ovyo huko Kibiti na Mkuranga zimerudi zote mkononi mwa dola na kusambaratisha mtandao wa kiuhalifu .
Aidha ametoa rai kwa wazazi na walimu kutoa taarifa kwenye vituo vya polisi mara watakapobaini kuna mwanafunzi mtoro ama hajaripoti shule kwa miezi kadhaa kwani wapo baadhi ya watoto wanaotumika kufundishwa uhalifu hata wakutumia silaha na watu wasiowema.
 
Pamoja na hayo IGP Sirro ,amesema vyombo vya ulinzi na usalama nchini vinashirikiana na nchi ya Msumbiji kupambana na wahalifu waliobainika kukimbilia nchini  humo wakitokea Tanzania.
 
Aliyasema hayo wilayani Kibaha ,mkoani Pwani ,katika ziara yake ya kikazi ya siku moja ambapo pia alizungumza na viongozi wa mashirika ya umma,wazee maarufu ,wastaafu mbalimbali na kamati ya ulinzi na usalama mkoani hapo.
 
IGP Sirro alieleza kuwa ,vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kupambana na yeyote atakaekuja kwa moto nae wataenda nae kwa moto na atakaekuja baridi wataenda nae baridi.
 
Alisema serikali imeshinda kwa hilo na hali kwa sasa ni shwari katika wilaya hizo.
 
IGP Sirro alieleza amepatiwa taarifa ya wanafunzi zaidi ya 1,300 mkoani hapo kuwa ni watoro na hawajulikani walipo hivyo wazazi washirikiane kusaidia jeshi la polisi kujua walipo.
 
“Kuna baadhi misikiti,makanisa yanadaiwa yanayotumia watoto hawa katika masuala ya kiuhalifu hivyo kuna kila sababu ya kuingia ndani kutafuta suluhu “
 
“Ni kazi yetu wazazi jamii na walimu kushirikiana ,na hapa ni muhimu wazazi wasaidie kusema watoto wao walipo ili kuwa na usalama” alisema .
 
Katika hatua nyingine IGP Sirro alielezea viongozi wa dini wana nafasi ya kuhakikisha wanatumia eneo lao kuhubiri amani .
 
“Tusidharau taarifa hata kama ni ndogo ,tusibweteke umoja ni nguvu tusaidiane kukomesha vitendo vya uvunjifu wa amani ” alifafanua IGP Sirro.
 
Akizungumzia changamoto ya wahamiaji haramu alisema wanashirikiana na uhamiaji kuusaka mtandao unaohusika kufanya biashara ya kusafirisha wahamiaji haramu .
 
IGP Sirro alisema hawatamvumilia yeyote anaekumbatia wahamiaji haramu kwani ni chanzo cha kusababisha kuleta magaidi  na kusafirisha bidhaa za haramu .
 
Alisema kwasasa wamejipanga kutaifisha mali za wafanyabiashara hao wa wahamiaji haramu na usafiri utaotumika kuwasafirisha.
 
Nae mkuu Wa Mkoa Wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,ameshukuru kuwepo Kwa kanda maalum kwani imeweza kuleta mafanikio makubwa .
 
Alisema kipindi cha nyuma kulikuwa na hali ya sintofahamu ,watu walisitiza shughuli zao za maendeleo ,biashara zilikwama,watu na baadhi ya viongozi walihama nyumba zao na wengine kulala saa 12 jioni kwa kuhofia mauaji.
 
Mhandisi Ndikilo alieleza sasa Kibiti na Rufiji hali ni shwarii kutokana na kuimarishwa ulinzi.
 
Aliwataka pia wawekezaji na wadau mbalimbali mkoani Pwani ,kujitokeza kushirikiana kusaidia kutatua changamoto zinazolikabili jeshi la polisi ikiwemo uhaba wa vitendea kazi ,usafiri na kujenga vituo vya polisi .
 
Mhandisi Ndikilo, alisema kuwa Mkoa huo umesheheni viwanda vya kutosha hivyo ni vyema kusaidia mambo hayo kwa manufaa ya wote wakati kukitokea uhalifu.
 
“Tukikumbwa na uhalifu tunapigia simu polisi, tusiwe Wa kwanza kulaumu wakati wa matatizo ,tukumbuke na kuwasaidia ili kufanikisha kazi zao kifanisi.;:” alisema mkuu huyo wa mkoa .
 
Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoani Pwani ,(ACP)Jonathan Shanna alisema ziara hiyo ni neema kwao na wamepewa maagizo mbalimbali ambayo watayafanyia kazi.
 
Kamanda Shanna alisema wamemfikishia kero IGP zinazowagusa askari polisi ikiwemo upungufu wa makazi .

No comments:

Post a Comment