WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro
kuwakamata, Bw. Bahman wa kampuni ya NAS na Wakala wa Kampuni ya
Wallmark Bw. Samwel kwa kutaka kutoa bandarini magari makubwa aina ya
semi tela 44 bila ya kulipa kodi kwa kutumia jina la Waziri Mkuu.
Pia
Waziri Mkuu ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA)
kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara
wanaotaka kukwepa kodi kwa madai ya kupewa vibali vya msamaha wa kodi
kutoka kwa viongozi wa juu Serikalini.
“Mtu
asije hapa aseme amepewa kibali na Rais Dkt. John Magufuli, Makamu wa
Rais Mama Samia Suluhu Hassan au Waziri Mkuu cha kutaka kutoa mzigo wake
bila ya kufuata taratibu. Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja
na achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.”
Ametoa
agizo hilo leo (Jumatano, Novemba 29, 2017) alipofanya ziara ya ghafla
bandarini baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara huyo aliyetaka
kuutapeli uongozi wa TPA kutaka kutoa magari hayo yaliyoingizwa nchini
mwaka 2015 kutoka nchini Uturuki.
Hatua
hiyo imekuja baada ya Bw. Bahman wa kampuni ya NAS kutaka kupata
msamaha wa kodi kwa kuidanganya TPA kwa madai kwamba wamewasiliana na
Waziri Mkuu na wasipotekeleza jambo hilo watapata matatizo.
Amesema
Serikali inasisitiza watu kufuata sheria na taratibu za nchi ikiwa ni
pamoja na kulipakodi ipasavyo na inataka watendaji wake wafanye kazi
bila ya kubugudhiwa, hivyo amewataka wafanyabiashara kufuata sharia za
nchi na kwamba Serikali haina ugomvi nao.
Waziri
Mkuu amefafanua kuwa mfanyabiashara huyo alitaka kuyatoa magari hayo
bila ya kukamilisha malipo ya ununuzi kutoka kwenye kampuni Serin ya
nchini Uturuki.
“Magari
haya aliyalipia asilimia 30 tu kwa makubaliano ya kumaliza asilimia 70
iliyobaki baada ya kufika Tanzania na atakapokamilisha ndipo angepewa
nyaraka ambayo inaonyesha jina la mwenye mzigo, aina ya mzigo na
thamani (bill of lading) inasaidia mteja kufanyiwa tathmini ya gharama
za kulipia ushuru, lakin huyu bwana hajafanya hivyo”
Waziri
Mkuu amesema kitendo cha kuyasajili magari hayo bila ya kuwa na nyaraka
hizo ni kinyume cha sheria na pia kinaweza kusababisha kampuni iliyouza
magari hayo ya Serin kutolipwa malipo yaliyobaki.
Amesema
jambo hilo halikubaliki kwa sababu linaweza kudhohofisha mahusiano
mazuri iliyopo kati ya Tanzania na Uturuki kwani tayari kampuni hiyo
imeshawasilisha malalamiko hayo katika ofisi za Ubalozi wa Uturuki
nchini Tanzania.
“Uturuki
wanawaamini sana wafanyabiashara wa Tanzania sasa huu ujanjaunja
uliotumika katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuyasajili magari
haya bila ya kuwa na bill of lading halisi unajenga sura mbaya kwa
wafanyabiashara wengine waaminifu na watiifu wa sheria nawaagiza TRA
kuchukua hatua kwa wahusika, hatuwezi kupoteza mahusiano na nchi kwa
sababu ya utapeli wa mfanyabiashara mmoja.”
Pia
Waziri Mkuu ametoa wito kwa Mawakala wa Forodha kuhakikisha wanakuwa
makini katika kazi zao na Serikali haitawavumilia wababaishaji kwani
inasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na si
vinginevyo.
Awali,
Mkurugenzi wa Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko alimueleza Waziri
Mkuu kuwa pamoja na vitisho vya mfanyabiashara huyo kuwa wasipotekeleza
matakwa yake watapata matatizo, lakini waliendelea kusimamia sheria na
taratibu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, NOVEMBA 29, 2017
No comments:
Post a Comment