Kwa
mara ya kwanza, Tundu Lissu amezungumzia shambulio la kinyama
alilofanyiwa na watu wasiojulikana kwa kueleza kuwa, alinusurika
kufumuliwa fuvu la kichwa kwa risasi.
Lissu,
Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Rais wa
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), aliyasema hayo jana, jijini
Nairobi anakotibiwa wakati akihojiwa na Jarida la Financial Times la
Uingereza.
Yakiwa
ni mahojiano yake ya kwanza tangu aliposhambuliwa nje ya makazi yake
yaliyoko Area D, mjini Dodoma Septemba mwaka huu, Lissu mmoja wa
wakosoaji wakubwa wa serikali alisema anaamini alikuwa mlengwa wa
jaribio la mauaji.
Akizungumzia
shambulio hilo dhidi yake, alisema sekunde chache baada ya watu wawili
wenye silaha kushuka katika gari lililokuwa likimfuatilia kwa wiki tatu,
derava wake alimsukuma chini ya sakafu ya gari lake wakati wakihangaika
kukwepa risasi nyingi zilizoelekezwa kwenye gari lake, nyingi zilimpiga
mgongoni na nyingine kwenye bega lakini risasi moja ilikosakosa kufumua
fuvu lake la kichwa.
“Hali
ikawa mbaya sana kwa sababu sikuweza kuhesabu risasi, naambiwa kwamba
risasi 38 zilipiga gari langu na 16 zilinipata na moja iliyokuwa
imelengwa kunifumua fuvu la kichwa ilinipiga begeni karibu na shingo,”
alikaririwa Lissu.
Mwanasiasa
huyo ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa kambi ya
upinzani alikakririwa akieleza zaidi kuwa kilichotokea ni ushahidi wa
kile ambacho amekuwa akikizungumzia mara nyingi kuhusu uwepo wa watu
waovu wanaotekeleza kampeni ovu ya kuipeleka nchi pabaya.
Wakati
Lissu akikutwa na mkasa huo mbaya, historia yake ya kisiasa inaonyesha
kuwa amekwishtakiwa mara sita, mwaka huu kwa makosa mbalimbali yakiwemo
ya uchochezi.
Wachambuzi
na wafuatiliaji wa mambo wamekuwa wakieleza kuwa shambulio hilo
linaweza kuwa moja ya mikakati ya magenge ya wapinzani wa serikali
waliobanwa na dola ambao sasa wanajaribu kutumia kila aina ya mbinu
kuifarakanisha jamii hususan wanasiasa.
Tayari
Jeshi la Polisi limekwishaanzisha uchunguzi wa tukio hilo na Inspekta
Jenerali (IGP), Simon Sirro amekwitoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa
zinazoweza kusaidia uchunguzi huo kuzitoa kwa makachero wa polisi.
Sambamba
na hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas naye alikutana na
waandishi wa habari kuzungumzia tukio hilo ambapo alitoa rai kuwa
shambulio hilo lisichukuliwe kisiasa kwa sababu ni uhalifu wenye sura za
ile ile ya matukio ya kihalifu ambayo yamekuwa yakitokea nchini.
Katika
mkutano wake na wanahabari alioufanya siku chache baada ya Lissu
kushambuliwa, Dk. Abbas alionya kuhusu upotoshaji uliokuwa ukifanywa na
baadhi ya watu waliokuwa wakijaribu kuipata matope serikali kwa
kuihusisha na shambulio na aliwataka wote wenye taarifa zinazoweza
kusaidia uchunguzi, akiwemo Lissu kutoa ushirikiano kwa polisi.
No comments:
Post a Comment