Tangu
kuanza rasmi Mei 10, 2016 kwa mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini
Dar es Salaam, zaidi ya nchi tano za Afrika zimetuma viongozi wake
kujifunza namna ya uendeshaji wake.
Mfumo
huo wa usafiri unalenga kupunguza foleni katika barabara, tangu
uzinduliwe na Rais John Magufuli nchi za Ethiopia, Malawi, Uganda na
Kenya zimetuma viongozi kuja kujifunza.
Pia,
ugeni kutoka Rwanda jana uliongeza idadi ya viongozi wanaoendelea kuja
mahsusi kwa ajili ya mradi huo huku kukiwa na taarifa za ujio mwingine
Desemba kutoka nchini Senegal.
Akielezea
utekelezaji wa mradi huo kwa wageni hao, mtendaji mkuu wa Wakala wa
Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Ronald Lwakatare kuwa wanatarajia
kuongeza mabasi kutoka 140 yaliyopo sasa hadi 305 katika awamu ya kwanza
ya mfumo huo itakapokamilika Juni mwakani.
Taarifa
iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Lwakatare, inasema wageni hao
sita kutoka Serikali ya Rwanda wana ziara ya siku tano kujifunza namna
wakala huo unavyotoa huduma.
Lwakatare
alisema ongezeko la mabasi kutasaidia kuongeza idadi ya abiria kutoka
200,000 wanaohudumiwa sasa kwa siku hadi kati ya 400,000 na 500,000.
“Licha
ya hilo, tutaongeza njia za mlisho kutoka mbili zilizopo sasa hadi tisa
zitakazokuwa zikienda Masaki, Sinza, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
maeneo mengine ambayo yapo jirani ili kupanua huduma ya usafiri kwa
maeneo yaliyomo ndani ya mfumo wa mabasi yaendayo haraka katika awamu ya
kwanza ya mradi,” alisema.
Kuhusu
athari zilizotokana na mvua iliyonyesha Oktoba 26, Lwakatare alisema
mabasi 20 yaliharibika zaidi lakini yameshatengezwa na yanatoa huduma.
Alisema
Dart imejipanga kuhakikisha mitaro yote inayozunguka karakana ya
Jangwani inasafishwa, ili kuepuka eneo hilo kukumbwa tena na mafuriko.
Naye
kiongozi wa ujumbe huo kutoka Mamlaka ya Halmashauri ya Jiji la Kigali,
Rwagatore Etienne alisema wamechagua kutembelea wakala huo kwa sababu
ndiyo mradi uliofanikiwa barani Afrika na upo karibu na Rwanda.
Katika
msafara huo, Etienne ameambatana na wataalamu washauri ambao waliopewa
kazi ya usanifu wa Jiji la Kigali ili liweze kuwa na mfumo wa mabasi
yaendayo haraka.
No comments:
Post a Comment