Katika
ajali hiyo iliyotokea katika kijiji cha Makomelo baada ya magari hayo
mawili kuvaana uso kwa uso watu 46 walijeruhiwa pia chanzo kikidhaniwa
kuwa mwendokasi wa lori.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Wilbroad
Mutafungwa alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa uchunguzi wa ajali
hiyo umeanza.
Alisema
katika uchunguzi huo, mmiliki wa Fuso hilo alipatikana mkoani Ruvuma na
kwamba jitihada za kumsafirisha zilikuwa zikiendelea.
Kamanda
Mutafungwa alisema aidha polisi inamsaka dereva na utingo wa Fuso hilo
ambao baada ya ajali hiyo walikimbilia kusikojulikana.
Aliahidi kuwasaka usiku na mchana na kuhakikisha wanapatikana popote walipo.
Kamanda
huyo aliwakumbusha madereva wote umuhimu wa kuendelea kutii sheria za
usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo na ulazima kwani ajali
zinapoteza nguvu kazi ya taifa.
Kufuatia
ajali hiyo, serikali tayari lishaagiza dereva atakayekematwa kwa kosa
la kuendesha kwa mwendokasi apelekwe mahabusu na kisha mahakamani,
kuanzia Alhamisi iliyopita.
Agizo
hilo lilitolewa bungeni Dodoma siku hiyo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mwigulu Nchemba, alipokuwa akitoa taarifa ya ajali hiyo.
Aidha,
Rais John Magufuli alilitaka Jeshi la Polisi, na kamati za ulinzi na
usalama za mikoa na wilaya kujitathmini na kutafuta majawabu ya ajali
katika salamu zake za rambirambi kufuatia ajali hiyo.
Basi
la City Boys lilikuwa likitoka Karagwe mkoani Kagera kwenda Dar es
Salaam kabla ya kugongana na Fuso lililokuwa linatoka Singida kwenda
Igunga.
Katika
taarifa yake, Waziri Mwigulu aliliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha
linamkamata na kumpiga faini dereva yeyote atakayeonekana anaendesha
gari kwa mwendokasi na asiachiwe hadi atakapofikishwa mahakamani.
Alisema mahakama ikijiridhisha kuwa ni kawaida ya dereva huyo kuendesha kwa mwendokasi, anyang’anywe leseni.
“Pia nasisitiza kila basi la abiria liwe na madereva wawili ili mmoja akikamatwa mwingine aendelee na safari,” alisema Mwigulu.
Waziri
huyo alilazimika kutoa kauli ya serikali bungeni baada ya Mwenyekiti wa
Bunge, Najma Murtaza Giga, aliyekuwa anaongoza kikao cha mchana,
kuitaka serikali itoe ufafanuzi kuhusu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa
Ulanga Mashariki, Goodluck Mlinga kuhusu ajali hiyo.
Mbunge
huyo wa CCM alidai ajali hiyo imetokana na ubovu wa barabara na kuitaka
serikali iwe inatoza faini kwa Wakala wa Barabara (Tanroads) pale ajali
zinaposababishwa na ubovu wa miundombinu kama ambavyo Jeshi la Polisi
linafanya kwa madereva wanaobainika kufanya uzembe barabarani.
Mlinga
alisema ajali ilisababishwa na shimo barabarani, hivyo ipo haja
Tanroads watozwe faini kwa kuwa wao pia wamekuwa wakitoza watu faini,
"wakati mwingine bila sababu".
Katika
taarifa yake, Waziri Mwigulu alikiri kuwapo kwa mashimo barabarani
kwenye eneo ilipotokea ajali hiyo lakini akasisitiza chanzo chake
hakikuwa mashimo bali mwendokasi wa dereva wa lori.
"Dereva
alikuwa anaendesha kwa kasi, alipokutana na lile shimo akaligonga lile
basi. Yale mashimo yaliyopo pale si ya kutisha na kutwa nzima magari
yaliyopita kwa mwendo wa kawaida hayakupata ajali," alisema.
Alisema
serikali imekuwa ikiwatoza faini madereva wanaofanya makosa barabarani
na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti ajali lakini sasa makosa ya
kuendesha kwa mwendokasi yamerejea tena na yanagharimu maisha ya watu.
"Naelekeza
Jeshi la Polisi popote pale watakaposhuhudia dereva anakwenda kasi
akamatwe, alipe faini na kuwekwa ndani kisha afikishwe mahakamani; na
ikibainika ana rekodi ya makosa afutiwe leseni," alisema.
No comments:
Post a Comment