Thursday, April 5, 2018

CHINA NA URUSI ZAUNGANA KUIKABILI MAREKANI.

UONGOZI wa Jeshi la China umeahidi kuisaidia na kuiunga mkono Urusi kijeshi kukabiliana na mataifa ya Magharibi dhidi ya mzozo wa kidiplomasia, vikwazo vya kiuchumi na mazoezi ya kijeshi.

Ahadi hiyo imetolewa Waziri wa Ulinzi wa China, Wei Feng ambaye yuko Urusi
kuhudhuria mkutano wa saba wa kimataifa wa usalama wa Moscow akiwa ameambata na ujumbe wa maofisa wa ngazi za juu wa jeshi.

Feng alisisitiza kwamba ziara yake imeratibiwa moja kwa moja na Rais wa China, Xi Jinping.

Alisema alikwenda Moscow akiwa na ujumbe maalumu kutoka kwa Jinping katika kipindi hiki ambacho mataifa yote mawili yanaboresha majeshi yao na ushawishi wao duniani licha ya wasiwasi wa Marekani.

“Naitembelea Urusi kama waziri mpya wa ulinzi wa China kuionyesha dunia maendeleo ya hali ya juu ya uhusiano wetu na dhamira imara ya majeshi yetu kuimarisha ushirikiano wa kimkakati,” alisema Wei wakati wa mkutano wake na Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergey Shoigu.

“Pili, kuisaidia Urusi kuendesha mkutano wa kimataifa wa usalama wa Moscow ili kuwaonyesha Wamarekani uhusiano wa karibu wa majeshi ya China na Urusi hasa katika hali ya sasa.

“Tumekuja kuwaunga mkono katika harakati zenu na hali inayowakabili,” aliongeza.

“Upende wa China uko tayari kuzungumza na Urusi kuhusu wasiwasi na misimamo yetu ambavyo vinawiana dhidi ya matatizo ya kimataifa katika majukwaa ya kimataifa pia,” alisema.

Hali hiyo inakuja huku mataifa hayo mawili yakiingia katika mzozo na Marekani katika maeneo tofauti kuanzia kijeshi hadi kiuchumi.

Rais Vladimir Putin wa Urusi na Jinping wa China wanaongoza kile kinachohesabiwa kuwa majeshi yenye nguvu yanayoshika namba mbili na tatu duniani nyuma ya Marekani.

Wakati Marekani imeendelea kuongoza kwa kipindi kirefu ikiwaacha kwa mbali washindani wake linapokuja suala la kijeshi, Moscow na Beijing zinakuja juu haraka zikilenga kuondoa pengo hilo na kudhibiti ushawishi wa Marekani katika siasa za dunia.

No comments:

Post a Comment