Tuesday, October 24, 2017

Ndoa za utotoni zakithiri Afrika Magharibi na Kati

bi harusi mtotoLicha ya kuwepo kwa upungufu wa kesi za ndoa za utotoni, nchi za Afrika Magharibi na Kati zimeshuhudia ongezeko la ndoa za utotoni.

Katika mkutano wa siku tatu ulionza Jumatatu huko nchini Senegal ulionuiwa kutokomeza ndoa za utotoni Afrika Magharibi na Kati, imebainika kwamba kwa wastani, binti mmoja anaezaliwa kati ya watatu katika eneo hilo ataolewa kabla ya miaka 18.
Idadi hiyo inafikia asilimia 76 nchini Niger.
Hali hii imeelezwa kuwa na athari kubwa katika elimu na afya ya wanawake na watoto, na vilevile kwa uchumi wa nchi, hii ni kwa mujibu wa Benki ya Dunia.
Siku ya kwanza ya mkutano huo, ambao ni wa kwanza kuwahi kufanyika nchini humo, washiriki wote wameonyesha kuwepo kwa dharura ya kutokomeza hali hiyo.
Mkutano huo unajumuisha mashirika ya kutoa misaada, mawaziri wa serikali mbalimbali, viongozi wa dini na wa jadi pamoja na viongozi kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Waziri mkuu wa Senegal Mohamed Dione amesem kinachotakiwa sasa hivi ni kutoka katika nadhari na kuelekea katika vitendo.
Kwa mujibu wa Al Hadj Sheikh Abu Bakar Conteh, mjumbe kutoka Baraza la Dini nchini Sierra Leone, viongozi wa dini watakuwa sehemu muhimu katika kutatua tatizo hilo.
"Wana jukumu kubwa sana katika kuwalinda na kuwatetea wafuasi wao dhidi ya kila kitu chenye madhara, kama hili tunalozungumzia, ndio maana, kwa sisi hapa Sierra Leon, mpango wowote wa kijamii ili ufanikiwe, ushirikishwaji wa viongozi wa kidini ni lazima," amesema Sheikh Abu Bakar Conteh.
Warsha na majadiliano yanaendelea mjini Dakar mpaka Jumatano.
Wanaharakati wanatumai kwamba mkutano huu utaleta mpango maalum na sheria, zitakazotokomeza ndoa za utotoni Afrika Magharibi na Kati kabla ya mwaka 2030.

No comments:

Post a Comment