Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amewaonya mawaziri na kuwataka watumie madaraka yao kwa manufaa ya Taifa na
kamwe wasiyatumie kama fursa ya kujitajirisha wao binafsi.
Kassim Majaliwa amesema hayo leo
Oktoba 16, 2017 alipozungumza na baadhi ya Mawaziri, Manaibu na Makatibu Wakuu
katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Aidha Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa
Rais Dkt. John Magufuli amesisitiza
kwamba amewateua ili wafanye kazi na kamwe
wasitumie madaraka waliyopewa kwa maslahi yao binafsi.
“Madaraka haya ya Uwaziri si fursa
ya kujipatia utajiri, tunatakiwa tufanye kazi kwa weledi, uadilifu, bidii na
uaminifu mkubwa ili kuondoa kero za wananchi kwa wakati.”
Waziri Mkuu amesema Mawaziri hao
wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka
kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. Pia utekelezaji wa ahadi zote zilizopo
kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 pamoja na ahadi alizozitoa Rais
Dkt Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka
Mawaziri hao wakapunguze urasimu katika utekelezaji wa malengo ya Serikali kwa
sababu wananchi wanahitaji kuhudumiwa kwa wakati
Mawaziri waliohudhuria kikao hicho
ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI Bw. Suileiman Jaffo pamoja na Manaibu
wake Bw. Joseph Kandege na Bw. George Kakunda, Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi Ummy Mwalimu na Naibu wake Dkt. Faustine
Ndungulile.
Wengine ni Waziri wa Maji na
Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe na Naibu wake Bw. Jumaa Aweso, Waziri wa
Viwanda na Biashara Bw. Charles Mwijabe na Naibu wake Mhandisi Stella Manyanya.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.
Hamisi Kigwangalla na Naibu wake Bw. Josephat Hasunga, Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako na Naibu wake Bw. William Ole Nasha,
Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Bw. Abdallah Ulega pamoja na Makatibu Wakuu wa
Wizara hizo.
No comments:
Post a Comment