Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema ana
mpango wa kupeleka bungeni maombi ya kuongezwa muda wa kustaafu maprofesa.
Amesema umri wa kustaafu kwa sheria
unawafanya wasomi hao washindwe kutumika vizuri kulijenga Taifa, hivyo ataomba
wastaafu wakiwa na umri wa miaka 65 badala ya 55.
Mkuchika amesema hayo leo Jumatatu
Oktoba 16, alipotembelea ofisi za
Sekretarieti ya Ajira na kukutana na
watendaji wa taasisi hiyo.
Amesema baadhi ya kada ambazo
zinafanyiwa kazi na maprofesa zinatakiwa kuangaliwa kwa jicho la tofauti.
Waziri amesema wengi wanapata
uprofesa wakiwa na miaka 55 na hufanya kazi kwa miaka michache na kutakiwa
kustaafu.
"Tutapeleka bungeni maombi kuwe
na mabadiliko kidogo katika baadhi ya maeneo, hawa maprofesa wengi wanaofikia
hatua hiyo wanakuwa na miaka kuanzia 50 na kuendelea halafu anafanya kazi
kidogo anatakiwa kustaafu," amesema.
Amesema haitakuwa na maana kama
wasomi hao wanatumia rasilimali za Taifa kufikia hatua hiyo halafu baada ya
kuhitimu wanafanya kazi kwa muda mfupi na kutakiwa kustaafu.
Mkuchika amesema pia atawasilisha
maeneo mengine ambayo yana upungufu unaotokana na sheria.
Amesema hayo akijibu changamoto
iliyotolewa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Xavier Daudi ambaye ameeleza
kuwa sheria inatoa mwanya kwa taasisi nyingine za umma kuajiri bila kupitia
sekretarieti hiyo.
"Kuna mgongano wa kisheria kati
ya sheria iliyoanzisha Sekretarieti ya Ajira na baadhi ya taasisi za umma
ambazo nazo zina mamlaka ya kuajiri watumishi kwenye taasisi zao," amesema
Daudi.
Akijibu hilo, Mkuchika amesema,
"Naahidi katika kipindi changu cha uwaziri nitafanyia kazi changamoto hiyo
na ikiwezekana maeneo yote yawekwe sawa kisheria."
Mkuchika amewaasa watendaji wa
taasisi hiyo kujiweka mbali na vitendo vya rushwa.
"Fanyeni kazi bila upendeleo,
jiwekeni mbali na rushwa natambua hakuna sehemu yenye changamoto ya rushwa kama
Sekretarieti ya Ajira. Usiombe faili lako lije kwangu eti mfanyakazi wa
sekretarieti ya ajira ana kesi ya rushwa," amesema.
Waziri amesema, "Nitasimamia
utendaji wa watumishi wa umma, tufanye kazi kulingana na malipo tunayolipwa na
kodi za Watanzania. Nafahamu wapo watumishi wa umma ambao wanalipwa mshahara
ilhali hawafanyi kazi inavyostahili."
Kuhusu watumishi wa umma
walioshiriki na kushinda katika uchaguzi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM),
amesema watawashughulikia kulingana na mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu
Kiongozi.
Amesema wakati nchi inaingia kwenye
mfumo wa vyama vingi, Katibu Mkuu Kiongozi alitoa mwongozo ambao ulielekeza
kuwa kuna baadhi ya watumishi wa umma kulingana na nafasi zao wapo
wanaoruhusiwa na wasioruhusiwa kushiriki kwenye siasa.
No comments:
Post a Comment