Monday, October 16, 2017

VIONGOZI NRM WAKATAA KUFUTWA UKOMO WA RAIS

Viongozi wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) mjini Buzaaya, Wilaya ya Kamuli mwishoni mwa wiki walipiga kura kupinga kufutwa ukomo wa umri wa rais kwenye Katiba.

Msimamo huo umekuja baada ya baraza la wazee kusema wabunge wanaoshinikiza
marekebisho ya Katiba ili kuondoa ukomo wa umri wa rais wanafanya hivyo ili kumfurahisha mtu mmoja tu.
Jukwaa la wazee hao limemkumbusha Rais Museveni ambaye atakuwa na umri wa miaka 77 ifikapo mwaka 2021 atakapokuwa anamalizi muhula wa sasa kwamba “muda umefika kwa yeye kupumzika ili kizazi kipya kichukue kuanzia alipoishia” na kuiendeleza nchi.

Kikao cha NRM
Uamuzi huo ulifikiwa na viongozi hao katika kikao cha kuomba ushauri wao kilichoandaliwa Jumamosi na mbunge wa Buzaaya, Isaac Musumba na kufanyika kwenye Chuo cha Ufundi cha Nawanyago.
Kikao hicho kililenga kupata maoni kutoka kwa wafuasi kindakindaki wa NRM kwa lengo la kuweka uzito katika marekebisho ya Katiba ambayo baadhi ya Waganda wanaona ni mkakati wa kumsafishia njia Rais Yoweri Museveni, 73, kuwania urais mwaka 2021 atakapokuwa na miaka 77.
Kikao hicho kilibadilika na kuwa cha mvutano wakati viongozi wa chama katika eneo hilo walipokuwa wanajaribu kuwazuia baadhi ya wanachama kufika eneo la kikao. Baadhi ya wanachama waliozuiwa kuingia kwenye kikao hicho walitishia kujiunga na vyama vya upinzani kwa maelezo NRM imeamua kuwaacha “yatima”
Ikiwa Katiba haitafanyiwa marekebisho, Rais Museveni hatakuwa na sifa ya kuwania kwa sababu ukomo wa umri kwa wagombea urais ni miaka 75.
“Rais Museveni alikwenda msituni kupambana dhidi ya madikteta waliong’ang’ania madarakani na aliahidi kurejesha demokrasia. Sasa anaathiriwa na mabadiliko ya msingi aliyoyafanya. Ni vema akijijengea heshima na urithi uliotukuka kwa chama cha NRM,” alisema Hamis Dheyongera, diwani wa Wankole (NRM).

No comments:

Post a Comment