Muungano
wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umeapa kujibu vikali shambulizi
la kombora lililofanywa jana na wapiganaji wa Houthi nchini Yemen kwenye
uwanja wa kiraia wa ndege kusini mwa Saudia na kuwajeruhi watu 23.
Muungano
huo, wa waislamu wa madhehebu ya Suni ambao umekuwa ukipambana na
vuguvugu la Kihouthi nchini Yemen linaloungwa mkono na Iran umesema
shambulizi hilo la mapema jana lilidhihirisha kuwa Iran inatoa msaada
kwa kile ulichokiita kuwa ni ugaidi wa nje ya mipaka.
Muungano huo ulisema kombora hilo lilipiga ukumbi wanakowasili abiria katika uwanja wa Abha, na kusababisha uharibifu.
Wahouthi
walisema katika vyombo vyao vya habari kuwa walifyatua kombora hilo na
kuupiga uwanja wa ndege wa Abha ulioko kusini mwa mpaka wa Yemen
unaotumika kwa safari za ndani na za kikanda.
No comments:
Post a Comment