Tuesday, June 18, 2019

Wabunifu wa umeme wa Njombe wakabidhiwa mamilioni yao na Tanesco kisa magufuli .


Shirika la umeme Tanzania Tanesco limewakabidhi kiasi cha shilingi milioni 30 (15mil kila mmoja) wabunifu wawili  wa umeme mkoani Njombe ili ziweze kuwasaidia katika kuboresha miundombinu yao.

Akizungumza wakati akikabidhi fedha hiyo mbele ya wananchi wa kijiji cha Lugenge kilichopo katika halmashauri ya mji wa Njombe mkoani humo,mkurugenzi mtendaji wa Tanesco DK.Tito Mwinuka amesema lengo la kufika katika kijiji hicho ni kutimiza ahadi waliyoitoa mbele ya Rais, huku akiahidi kushirikiana na wabunifu hao ili kuongeza nguvu ya umeme katika vijiji vya wabunifu hao.

“Kama tulivyo ahidi tulituma wataalamu wamefika hapa tangu juzi na wameweza kubaini,ni vitu gani vikifanyika basi vinaweza kusaidia ule umeme upatikane mwingi zaidi  na wananchi waweze kufaidika,kwa hiyo kwa maeneo hayo mawili tumeona kuna uwezekano wa sisi Tanesco kusaidia umeme kupatikana mkubwa zaidi kule msete na hapa Lugenge,uwe salama zaidi na watu waweze kufaidika”alisema Dkt.Mwinuka

John Fute maarufu kwa jina la mzee Pwagu mbunifu wa umeme katika kijiji cha Msete unaozalisha  kilowati 28, mara baada ya kupokea fedha kiasi cha shilingi milioni 15 ametoa rai kwa wananchi kuendeleza vipaji vya watoto wao.

“Mimi langu moja kila mtoto amezaliwa na kipaji chake sasa niwaombe wazazi wenzangu, tujaribu kuwasaidia watoto sio kuwafifisha unaweza kuona siku moja umefanikiwa mfano kama mimi sasa hivi nina miaka 60 lakini nimeanza tangu mwaka 1980 kutengeneza umeme”

Kwa upande wake Lainery Ngailo mbunifu wa umeme katika kijiji cha Lugenge unaozalisha kilowati 15 ameishukuru serikali kwa kuwafikisha wataalamu katika kijiji chake na kuahidi kushirikiana nao ili kuwafikishia nishati wananchi.

Aidha shirika hilo limemkabidhi shilingi milioni moja na laki nne mwandishi wa habari wa  shirika la utangazaji Tanzania TBC Tatu Abdalah kazimoto kwa kuwaibua wabunifu hao.

Nao baadhi ya wananchi katika kijiji cha Lugenge akiwemo bwana John mfyagindza wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania dkt.John Pombe Magufuli kwa kuwaona wataalamu hao kutokana na kuwepo kwa wataalamu wengi vijijini wanaoweza kufanya mambo makubwa lakini wamekuwa wakikosa ushirikiano na baadhi ya taasisi za serikali.

June 13 shirika hilo liliahidi kutoa fedha hiyo kwa wabunifu hao mbele ya Rais Magufuli katika kikao cha wabunifu wa uzalishaji wa umeme nchini kilichofanyika Ikulu jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment