Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameuagiza uongozi wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro uwaruhusu wananchi wa Kata ya Alaitole
wajenge shule ya wasichana ya bweni katika eneo la Esere lililo ndani
ya Mamlaka hiyo ili waweze kupata elimu kufuatia wananchi hao kuzuiwa
kwa muda mrefu kutekeleza mradi huo.
Aidha,
ameutaka uongozi wa Mamlaka hiyo utoe kibali cha kuwawezesha wananchi
kata hiyo kuanza ujenzi haraka iwezekanavyo ili fedha zilizotolewa na
Serikali shilingi milioni 298 zianze kutumika.
Dkt.
Kigwangalla ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na kusikiliza
kero za wananchi wa Kata Alaitole wilayani Ngorongoro kwenye mkutano wa
hadhara uliowashirikisha viongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,
viongozi serikali wa kata hiyo, viongozi wa mila wa kabila la Masai na
madiwani na Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mhe. William Ole Nasha.
Amesema
Serikali inaunga mkono juhudi zote za wananchi za kujiletea maendeleo
akifafanua kwamba hatua ya wananchi hao kuamua kujenga shule ya
Sekondari ya Bweni ni jambo la linalopaswa kupongezwa na kila mpenda
maendeleo.
“Mnacho
kitaka kiko wazi, mnataka maendeleo ya watoto wenu, katika hili mmesema
kila baba anatoa elfu hamsini na wanawake wanatoa elfu ishirini, hili
ni jambo kubwa achilia mbali nguvu kazi mnayojitolea na tayari serikali
imeshaleta milioni 298, haiingii akilini eneo linalochangia kuleta na
kuingiza mapato mengi Serikalini kiasi cha bilioni 126 likose shule”
Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.
Dkt.
Kigwangalla ameeleza kuwa ujenzi shule hiyo utawaondolea wanafunzi adha
ya kutembea umbali mrefu akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuwaunga
mkono wananchi hao kwenye mipango yao ya utekelezaji miradi ya
maendeleo.
Amesema
jamii hiyo pamoja na mazingira wanayoishi kuwa ndani ya Hifadhi ya
Ngorongoro wanahitaji elimu. Aidha, amesema pia ni muhimu katika sekta
ya utalii kupitia utamaduni wao akiongeza kuwa kazi ya Wizara ni kuona
mafanikio ya sekta ya utalii yanakuwa kwa kuongeza mapato na sio
migogoro.
Dkt.
Kigwangalla amesema Hifadhi ya Ngorongoro ni hifadhi mseto inayoruhusu
binadamu na wanyama kuwepo katika eneo moja na kwamba hiyo ipo kwa
mujibu wa sheria akiitaka Mamlaka hiyo kuyatazama vizuri majukumu yake
ya kuendeleza Utalii, Kulinda rasilimali zililizopo kwa maana ya
kuhifadhi na kuhudumia jamii iliyo ndani ya hifadhi hiyo.
Katika
hatua nyingine ameutaka uongozi wa Mamlaka hiyo uendelee kufanya
mazungumzo na wananchi hao badala ya kujielekeza katika matumizi ya
nguvu ili kupata uelewa wa pamoja akitolea mfano wa eneo la Loliondo
ambalo hivi sasa lina utulivu.
“
Viongozi wa Mamlaka mnalo jukumu la kuwasikiliza wananchi na kuamua kwa
pamoja, eneo la Ngorongoro ni Urithi wa dunia na litaendelea kuwa hivyo
kwa kuheshimu na maslahi ya Taifa na maslahi ya walio walio wengi”
Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.
Kuhusu
mahusiano baina ya wananchi na wahifdhi Dkt. Kigwangalla amesema kuwa
kupitia mkutano wake na wananchi amebaini kuwepo kwa tatizo la
mawasiliano na mahusiano baina ya wananchi wa eneo hilo na watumishi wa
Serikali walio chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro akibainisha
kwamba tayari serikali imeliona jambo hilo na inaendelea kulifanyia
kazi.
Naye
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa
jimbo la Ngorongoro Mhe. William Ole Nasha akizungumza wakati wa mkutano
huo amempongeza na kumshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.
Hamisi Kigwangalla kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha ulinzi wa
rasilimali za Taifa katika maeneo mbalimbali nchini.
Amemwomba
aeendelee kutembelea maeneo mengine ya jimbo hilo kwa lengo la
kusikiliza kero za wananchi wa kata za wilaya hiyo kwa lengo la
kudumisha mahusiano mema.
Mhe.
Ole Nasha ameeleza kuwa hatua ya Wizara kutafutia ufumbuzi mgogoro huo
wa ujenzi wa shule ya wasichana ya bweni, vile vile uamuzi wa serikali
kutoa eneo na fedha kiasi cha shilingi milioni 298 kwa ajili ya ujenzi
wa shule hiyo katika eneo lililokubaliwa ni ishara tosha kwamba Serikali
inawalinda na kuwajali wananchi wake.
Amesema
wananchi wa jimbo la Ngorongoro pamoja na changamoto mbalimbali
zinazowakabili wako ni wasikivu na wako tayari muda wote kushirikiana na
Serikali ikiwemo ulinzi wa rasilimali zilizopo na kuendeleza uhifadhi
katika hifadhi ya Ngorongoro.
Kwa
upande wao wananchi wa Kata ya Alaitole wakizungumza kwa nyakati
tofauti wamemshukuru Dkt. Kigwangalla kwa kuamua kuwafuata na kuzungumza
nao katika makazi yao wakimpongeza kwa juhudi zake za kutatua
changamoto mbalimbali kwa maslahi ya wananchi na uhifadhi.
Aidha,
wamemwomba kuendelea kuisimamia sekta ya uhifadhi nchi wakitoa wito wa
kudumisha mahusiano mema baina ya wananchi na wahifadhi.
By Rich Voice
No comments:
Post a Comment