Meneja wa Arsenal Arsene Wenger
alipoteza fursa pekee ya kushinda kombe msimu wake wa mwisho akiwa
katika klabu hiyo baada ya kuchapwa na Atletico Madrid katika nusu
fainali ya ligi ndogo ya klabu Ulaya Europa League.
Arsenal walishindwa kwa jumla ya mabao 2-1.
Mechi ya mkondo wa kwanza, matokeo yalikuwa 1-1 lakini kwenye mechi ya Alhamisi iliyochezewa Madrid, mshambuliaji wa zamani wa Chelsea Diego Costa alirejea kuwaadhibu Gunners alipofunga bao dakika za mwisho mwisho za kipindi cha pili (dakika ya 45+2).
Kwa bao hilo, Costa alifuta matumaini ya Arsneal ya kushinda kombe msimu huu na kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.
Bao la Costa lilitokana na pasi muhimu kutoka kwa mshambuliaji Mfaransa Antoine Griezmann ambaye amekuwa akitafutwa na klabu kadha kuu Ulaya.
Ulikuwa usiku usio wa bahati kwa Arsenal kwani nahodha wao Laurent Koscielny aliondolewa uwanjani kwa machela baada ya kuumia kwenye kano za sehemu ya nyuma ya kifundo cha mguu.
Jeraha hilo huenda likamfanya Mfaransa huyo kutoshiriki Kombe la Dunia mwezi ujao.
Baada ya kushindwa, Arsenal sasa hawatashiriki Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa msimu wa pili mfululizo.
Wenger, ambaye ataondoka klabu hiyo mwisho wa msimu huu baada ya kuwaongoza kwa miaka 22, hajashinda kombe lolote la ubingwa Ulaya akiwa katika klabu hiyo.
Wenger hataondoka kwa shangwe alivyotaka
Wenger alikuwa amesema alitaka kuhitimisha "hadithi ya mapenzi yake na Arsenal" vyema kabla ya mechi hiyo lakini sasa amenyimwa fura hiyo baada ya kufungwa mechi yake ya 250 akiwa na Arsenal barani Ulaya.Licha ya kushinda Ligi ya Premia mara tatu na Kombe la FA mara saba, Gunners wamefika fainali za Ulaya mara mbili pekee katika misimu 21 ambayo walishiriki mashindano hayo wakiwa wa Wenger.
Walishindwa na Galatasaray kwa mikwaju ya penalti katika fainali ya Kombe la Uefa 2000 na walilazwa 2-1 na Barcelona katika fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mwaka 2006.
Mechi ya mwisho kwa Mfaransa huyo akiwa na Arsenal ligini itakuwa ugenini dhidi ya Huddersfield 13 Mei.
Wenger alisema nini baada ya mechi?
Akizungumza na BT Sport meneja wa Arsenal Arsene Wenger alisema: "Ilikuwa ni mechi sawa tu na tuliyokuwa nayo mkondo wa kwanza. Nafasi nzuri tulizoziunda zilikuwepo lakini tulikosa kumakinika. Tulicheza dhidi ya timu nzuir na nawatakia kila la heri kwenye fainali lakini tunahisi kwamba tulifanya yote tuliyohitaji kufanya kufika fainali."Hatukuweza kudhibiti matukio muhimu zaidi kwenye mechi zote mbili vyema. Tulikuwa 1-0 mbele dakika kumi kabla ya mechi kumalizika nyumbani, kisha tukafungwa bao la kijinga. Leo tulionekana sawa lakini tulifungwa baada yao kujibu shambulizi.
Atletico walicheza kwa woga kipindi cha kwanza kwamba tungefunga wangetolewa, lakini walipofunga walicheza wakijua kwamba wana nafuu. Tuliupoteza mpira na Diego Costa ni mmoja wa mastraika wazuri zaidi duniani."
Kuhusu kuumia kwa Laurent Koscielny, Wenger alisema: "Ni jeraha la misuli ya sehemu ya nyuma ya mguu na pengine tutakuwa na habari njema, lakini dalili za kwanza si nzuri."
Alipoulizwa kuhusu mwisho wa safari kwa Arsenal Ulaya, alisema: "Inauma sana lakini ni lazima upitie haya katika mchezo huu. Unaweza kuwa mchezo katili lakini wakati mwingine ni mzuri. Tumeumia sana leo kwa kweli."
Costa kuwaadhibu Arsenal
Kulikuwa na hisia fulani za machungu Costa alipoutuma mpira wavuni muda wa ziada kabla ya mapumziko.Mhispania huyo aliwasumbua sana Gunners alipokuwa Chelsea - zaidi Septemba 2015 aliposababisha kufukuzwa uwanajni kwa wachezaji wawili wa Arsenal.
Alikuwa tishio kwao Madrid tangu mechi ilipoanza, alifanikiwa kumkwepa Nacho Monreal wa Arsenal mwanzoni na kujiundia nafasi ambayo nusura afunge bao lake la kwanza.
Wakati huo alionekana kutotulia na mpira wake ukapaa juu ya mwamba wa goli lakini baadaye alimakinika zaidi.
Alishirikiana vyema zaidi na Griezmann na kuwasumbua Arsenal sana katika kujibu mashambulizi, yaani kaunta.
Costa alikaribia kusaidia ufungaji wa bao alipompa mpira Griezmann lakini Calum Chambers akamzuia Mhispania huyo.
Alikuwa pia na utukutu wake, na alizozana na Shkodran Mustafi uwanjani na wote wawili wakapewa kadi za manjano.
Arsenal mwishowe waliadhibiwa kwa nafasi nyingi walizopata na kushindwa kufunga na pia kwa kufungwa bao la ugenini dakika za mwisho mechi ya kwao nyumbani. Walikuwa wamecheza dhidi ya wachezaji 10 kwao Emirates kwa dakika 80 lakini walifunga bao moja pekee kutoka kwa makombora 28 waliopiga kulenga goli licha ya kwamba pia waliudhibiti mchezo kabisa.
Madrid, Alexandre Lacazette alisita alipopewa mpira mzuri na Aaron Ramsey kipindi cha kwanza na Monreal baadaye alimkosea kwa kutodhibiti mpira vyema.
Granit Xhaka alijaribu kufunga kutoka mbali lakini kipa Jan Oblak akautema mpira. Henrikh Mkhitaryan naye alirusha kombora lakini likatikisa wavu kutoka nje.
Beki wa Atletico Diego Godin alikuwa anazuia karibu kila mpira uliokuwa unajaribu kupitishwa eneo lake. Aliwazuia Mesut Ozil, Ramsey na Hector Bellerin kupenya.
Matokeo yaArsenalkatikaEuropa League 2017-18 | |
---|---|
Arsenal 3-1 Cologne (hatua ya makundi) | Bate Borisov 2-4 Arsenal (hatua ya makundi) |
Red Star Belgrade 0-1 Arsenal (hatua ya makundi) | Arsenal 0-0 Red Star Belgrade (hatua ya makundi) |
Cologne 1-0 Arsenal (hatua ya makundi) | Arsenal 6-0 Bate Borisov (hatua ya makundi) |
Ostersunds FK 0-3 Arsenal (32bora mkondo wa kwanza) | Arsenal 1-2 Ostersunds FK (32bora marudio) |
AC Milan 0-2 Arsenal (l16mkondo wa kwanza) | Arsenal 3-1 AC Milan (16bora marudio) |
Arsenal 4-1 CSKA Moscow (robo fainali mkondo wa kwanza) | CSKA Moscow 2-2 Arsenal (robo fainali marudio) |
Arsenal 1-1 Atletico Madrid (nusu fainali mkondo wa kwanza) | Atletico Madrid 1-0 Arsenal (nusu fainali marudio) |
CHANZO-BBC SWAHILI |
No comments:
Post a Comment