Friday, March 23, 2018

Bara la Afrika Kugawanyika Mara Mbili


Wanajiolojia wameeleza kwamba Tanzania na baadhi ya nchi nyingine za Afrika, zitameguka na kuwa visiwa.

Hata hivyo, wamesema mchakato huo utachukua mamilioni ya miaka.

Wamesema kuibuka kwa ufa mkubwa katika eneo la Bonde la Ufa, Kusini Magharibi mwa Afrika kutasababisha nchi za Kenya, Tanzania, Djbouti na Msumbiji kumeguka.

Pamoja na hayo, mjiolojia mwandamizi wa Wakala wa Jiolojia Tanzania, Gabriel Ndogoni alisema  kuwa kumeguka huko kutasababisha baadhi ya nchi za Afrika ambako Bonde la Ufa linapita kuzungukwa na bahari.

“Zitakuwa kama ilivyo kwa visiwa vya Madagascar au Zanzibar,” alisema.

Ndogoni alisema kwa waliosoma Jiografia, mchakato huo ni kama ule wa kugawanywa kwa mabara saba, “Zile nguvu za kupasuka kwa miamba hadi yakawepo mabara saba duniani bado zinaendelea. Mkondo huu wa Bonde la Ufa, ulianzia Kaskazini mwa Afrika katika nchi za Djibouti, Kenya mpaka Kusini mwa Tanzania.”

Alisema mkondo wa kwanza upo Ethiopia na kwa upande wa Kenya kuna miwili ambayo mmoja ndio uliopita hadi katika baadhi ya maeneo ya Tanzania kama Manyara, Singida, Iringa na Mbeya.

Alisema kasi ya maeneo hayo kujitenga ni milimita 0.1 Kusini mwa Afrika na milimita 6.5 Kaskazini mwa Afrika na kwamba Tanzania ipo katikati ya maeneo hayo.

“Kumeguka huku kwa bara la Afrika kunaleta wasiwasi kwa sababu kunatokea katika makazi ya watu,” alisema.

Dk James Hammond wa Idara ya Sayansi na Uhandisi kutoka Chuo cha Imperial cha London alinukuliwa na jarida la mtandaoni la Mail & Guardian akisema, “Katika miaka milioni kadhaa ijayo, shughuli hii itakamilika na kuigawa Afrika mara mbili, na kuunda bahari mpya hapo katikati. Ukitumia jiografia ya sasa, bara hilo jipya litashirikisha Somalia, nusu ya Ethiopia, Kenya na Tanzania.”

Baadhi ya wanajiolojia wanakadiria kwamba huenda mpasuko huu ukayabeba pia mataifa ya Uganda, Rwanda, Burundi na maeneo ya Malawi na Msumbiji.

Hivi karibuni, maofisa wa Mamlaka ya Taifa ya Barabara Kenya (KeNHA) wakishirikiana na mkandarasi kutoka China anayejenga reli ya kisasa, walifika katika bonde hilo kuziba baadhi ya nyufa.

Baada ya uchunguzi, ilibainika kwamba hali hiyo ilitokana na shughuli ya kijiolojia chini ya ardhi ambayo ilihusisha mvutano wa vipande vikubwa vya ardhi.

Siku chache baadaye, ufa huo uliendelea kupanuka na kuathiri barabara hiyo tena jambo lililosababisha magari yenye kubeba mizigo mizito kushindwa kupita. Pia ufa huo ulianza kuathiri nyumba za wakazi.

“Mkandarasi na wahandisi wako hapo kwa sasa na watabaki ili kufuatilia yanayojiri kutokana na shughuli za kivolkano ambazo zilisababisha ufa huo,” naibu mkurugenzi wa mawasiliano wa Kenya, Charles Njogu alisema baada ya ukarabati huo mara ya kwanza.

No comments:

Post a Comment