SERIKALI
ya Ufaransa imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa mapambano dhidi ya
rushwa na inaamini fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
mbalimbali zitatumika kama ilivyokusudiwa.
Kauli
hiyo imetolewa jana (Jumatatu, Machi 05, 2018) na Balozi wa Ufaransa
nchini Tanzania, Bw. Frederic Clavier alipomtembelea Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Balozi
Clavier alisema Ufaransa imeridhishwa na mapambano ya rushwa
yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John
Magufuli wataendelea kushirikiana nayo katika uboreshaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo.
Pia
Balozi huyo alisema Septemba mwaka huu wanatarajia kufungua ofisi ya
Shirika la Kimataifa la Misada ya Maendeleo la Ufaransa (AFD) jijini Dar
es Salaam ili kurahisisha utoaji wa huduma.
Kwa
sasa ofisi za AFD zipo Nairobi nchini Kenya.Shirika hilo limekuwa
likishirikiana na Serikali, katika utekelezaji wa miradi mbalimbali
ikiwemo na ya maji safi na maji taka kwenye mikoa ya Simiyu, Mwanza,
Musoma na Morogoro.
Kwa
upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Serikali imeweka
kipaumbele katika uwajibikaji na kupambana na rushwa ili kuhakikisha
fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi zinatumika vizuri
pamoja na wananchi kupata haki.
Alisema
mapambano dhidi ya rushwa yataiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya
kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda, uwekezaji, kilimo na utalii,
hivyo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini
Ufaransa ili waje kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda, kilimo, madini na
miundombinu mbalimbali.
Pia
Waziri Mkuu alisema Serikali itashirikiana na Ufaransa katika kuandaa
mikutano mbalimbali itakayowakutanisha wadau wa sekta binafsi kutoka
nchi zote mbili ili kuwapa mbinu za namna ya kukuza uchumi.
No comments:
Post a Comment