Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi amesema Serikali imefanyia mabadiliko Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuanzisha Ofisi nyingine mbili mpya kwa lengo la kuongeza Tija na Ufanisi katika utendaji kazi.
Prof Kabudi alikuwa akizungumza na watendaji wa Wizara na Taasisi zinazounda sekta ya Sheria nchini makao makuu ya Wizara mjini Dodoma ambao
wanakutana mjini humo kujadili na kuandaa makadirio ya Bajeti ya Wizara na Taasisi zake.
wanakutana mjini humo kujadili na kuandaa makadirio ya Bajeti ya Wizara na Taasisi zake.
Prof. Kabudi amesema uundwaji wa Ofisi mbili mpya za Ofisi ya Taifa ya Mashitaka na Ofisi ya Wakili Mkuu unafanya sasa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kubaki na jukumu lake la msingi la kuishauri Serikali katika masuala yote ya kisheria, kufanyia uhakiki mikataba ya kitaifa na kimataifa na kuratibu wanasheria wote walioko katika Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Wakala, Mamlaka, Mashirika ya Umma na Serikali za Mitaa.
Amesema Ofisi ya Taifa ya Mashitaka sasa itajikita katika uendeshaji wa mashitaka ya jinai mahakamani ikiwa na wanasheria wake wakati Ofisi ya Wakili Mkuu kupitia wanasheria wake itajikita katika uendeshaji wa mashitaka ya madai ya kitaifa na kimataifa, utatuzi wa migogoro kitaifa na kimataifa na ushughulikiaji wa mikataba ya kitaifa na kimataifa ambayo taasisi za umma zinaingia kwa niaba ya nchi.
Amewataka watumishi wa umma ambao ni wanasheria kuwa tayari na kujipanga kutokana na mabadiliko hayo ambayo yatasababisha uhamisho wa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ili kuyatekeleza kwa vitendo yale yote yanayotarajiwa kupatikana baada ya mabadiliko hayo.
Amesema serikali imefikia uamuzi huo ili kuweza kufanikisha azma ya kuwaweka pamoja wanasheria wote na kuwaratibu ili kujua nani yuko wapi na anafanya nini n a kuongeza kuwa wanasheria hao sasa watawajibika kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye atakuwa na jukumu la kumpeleka mwanasheria yoyote atakayemuona anafaa kufanikisha jambo jema la Serikali.
“Wakuu wa Idara na Vitengo vya Sherioa katika mashirika makubwa ya umma na ambayo Serikali imetoa mabuiloni ya fedha zake ili kuyaendesha wataangaliwa na mwanasheria mkuu na kama akionekana hakamilishi lengo la kuwepo katika ofisi husika basi mara moja atapelekwa mwingine mwenye uwezo wa kuisadia Serikali,” alisema Prof Kabudi.
Akizungumza katika kikao hicho Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Alderaus Kilangi amewataka watendaji wa ndani ya Sekta ya Sheria kufanya kazi kama timu moja ili kuweza kurejesha imani ya wananchi kwa wataalamu wa sekta hiyo ambayo inapaswa kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
“Niwaombe wanasheria wenzangu tuwe timu moja na tufanye kazi zetu kwa weledi na ufanisi mkubwa ili kuhakikisha maendeleo ya kweli ya nchi yanafikiwa, ni kweli kama sekta tulianza kupoteza mwelekeo, tuyachukulie maboresho haya ya miundo ya Ofisi zetu kama chachu ya kuleta tija na ufanisi katika kazi zetu,” alisisitiza
Mkutano huo ulihudhuriwa na watendaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mahakama ya Tanzania, ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume ya Kurekebisha Sheria,Wakala wa Ufilisi na udhamini (RITA), Tume ya Utumishi wa Mahakama, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo( Law School) Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto.
No comments:
Post a Comment