TAARIFA KWA UMMA
UFAFANUZI WA HOJA ZA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI (NEC) DHIDI YA TAMKO LA ASASI ZA KIRAIA
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimepokea barua Kumb. Na.
BA.71/75/01/124 ya tarehe 22 February 2018 kutoka kwa Mkurugenzi wa
Uchaguzi Ndugu Kailima Ramadhani na kupitia kwa umakini mkubwa hoja za
Tume Ya Uchaguzi dhidi ya tamko lililotolewa na umoja wa Asasi Za
Kiraia, chini ya Jukwaa la Wakurugenzi wa AZAKI, Februari 21, 2018
kuzungumzia hali ya usalama wa raia, haki za binadamu na utawala wa
sheria hapa nchini.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kama moja ya asasi zinazounda umoja wa
AZAKI hizo kimelazimika kujibu hoja hizo kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi
katika tamko lake lililotolewa Ijumaa Februari 23, 2018 imekituhumu
moja kwa moja Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kupitia kwa aliyekuwa
Kaimu Mkurugenzi, Bw. Paul Mikongoti, kwa kutoa tamko lenye tuhuma za
kupotosha baadhi ya mambo kupitia tamko hilo la umoja wa AZAKI.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kinapenda kutanguliza pongezi kwa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi kwa kupitia hoja pamoja na mapendekezo yaliyotolewa
na asasi za kiraia nchini na hata kutoa kasoro za uwasilishaji wa
baadhi ya hoja hizo.
Hata
hivyo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinapenda kuikumbusha Tume
kwamba, tamko husika halikutolewa na Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu bali tamko hilo lilitolewa na Umoja wa AZAKI chini ya Jukwaa la
Wakurugenzi wa AZAKI.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kilishiriki kwenye tamko hilo kama
mwanachama wa AZAKI kwa kutambua wazi kuwa lengo la tamko hilo ni
kuimarisha hali ya haki za binadamu na demokrasia nchini na si
vinginevyo. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinapenda kuitoa
wasiwasi Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa hakuna maslahi tofauti wala
upotoshaji wa makusudi katika utoaji wa tamko hili.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kinakiri kufahamu kwa kina sheria na
kanuni zinazoratibu chaguzi na kinatambua kwamba lengo la AZAKI haikuwa
kubeza wala kuvunja kanuni hizo bali kutoa mapendekezo kwa ajili ya
maboresho ya chaguzi na hatimaye kuimarisha demokrasia nchini Tanzania.
Hata
hivyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimesikitishwa na kitendo
cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kumshambulia moja kwa moja Bw. Paul
Mikongoti licha ya ukweli kwamba, Bw. Paul Mikongoti alikiwakilisha
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kama mwanachama wa umoja huo wa
AZAKI.
Kituo
kinapenda kuifahamisha Tume kuwa tamko hili la AZAKI lilisomwa na
wakurugenzi tofauti maeneo tofauti nchi nzima na hivyo haikuwa busara
kwa Tume kumshambulia moja kwa moja Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu wala Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa
ubinafsi wake.
Ingawa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi haikuwa sahihi kukituhumu Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Paul
Mikongoti, bado Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeonelea ni
busara kufafanua hoja zilizotolewa na umoja wa AZAKI kama ifuatavyo:
1. Kuhusu kituo cha televisheni cha ITV kuadhibiwa na kutakiwa kuomba radhi kwa kurusha habari za kuibwa kwa sanduku la kura
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kinapenda kuijuza Tume ya Uchaguzi kuwa
kilikubaliana na hoja hii iliyotolewa na umoja wa AZAKI kwa kuzingatia
misingi ya uhuru wa vyombo vya habari kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya
Katiba Tanzania inayotoa haki kwa kila Mtanzania pamoja na vyombo vya
habari kutafuta na kupokea habari mahali popote pale bila kujali mipaka
ya nchi.
Hata
hivyo baada ya kupitia hoja hii kama ilivyofafanuliwa na Tume ya
Uchaguzi, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaishauri Tume
kuboresha kanuni za usimamizi wa uchaguzi ili kutokuweka mipaka kwa
vyombo vya habari kwa kuzingatia kwamba vyombo vya habari vinatoa
taarifa kwa maslahi ya umma.
2. Kuhusu mashirika mbalimbali kunyimwa kibali cha uangalizi wa uchaguzi
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kilikubaliana na hoja hii kwa kuzingatia
malalamiko yaliyotokana na AZAKI ya PACUSO ambao walikiri kupata majibu
kutoka Tume kuwa tayari nafasi zimejaa.
Hata
hivyo baada ya kupitia hoja hii ya Tume, Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu kinaishauri Tume ya Uchaguzi kuboresha utaratibu wa maandalizi
kuelekea uchaguzi ili kutoa nafasi kwa asasi zenye lengo la kufanya
uangalizi kufurahia haki hiyo bila kuhisi uwepo wa kuzuiliwa. Moja ya
maboresho hayo ni kuweka muda wa kutosha wa kutuma maombi na kuweka
nguvu katika kufikisha taarifa kwa mashirika na wadau wengine. Kufuatia
ukweli kwamba Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ndio asasi pekee
iliyopata kibali kutazama uchaguzi huu, hili lilipelekea butwaa kwa
umoja wa AZAKI kwa kulinganisha na chaguzi zilizopita.
3.
Tume kuweka utaratibu mpya unaowataka watazamaji kuwasilisha taarifa
hizo ili zikaguliwe, kuangalia yaliyomo na kuridhiwa na Tume
ikiipendeza.
Katika
hoja hii, Kituo kinaungana na AZAKI kuhoji umuhimu wa utaratibu
ulioanzishwa na Tume mwaka 2015 wa AZAKI kusubiri hadi Ripoti ya awali
ya uangalizi iwasilishwe kwa Tume, na Tume kukiri kupokea ripoti hiyo
ndipo AZAKI zinazoangalia uchaguzi kuweza kutoa kwa umma taarifa za
uangalizi. AZAKI zimeonelea kwamba utaratibu huu unafifisha misingi ya
uhuru wa asasi za kiraia katika uangalizi wa uchaguzi.
Utaratibu
huu pia umelalamikiwa kwa kuzingatia kuwa Tume haijaweka muda maalumu
ambao itatumia kabla ya kukiri kupokea ripoti ya uchaguzi.
Utaratibu
huu umelalamikiwa na AZAKI kuwa kwa upande mwingine unaondoa dhana ya
AZAKI kuwa vyombo huru vya uangalizi wa uchaguzi.
Mwisho
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaishauri Tume ya Uchaguzi
kuzishirikisha asasi za kiraia na wadau wengine muhimu katika maboresho
ya sheria, kanuni na taratibu zinazoratibu utendaji wa Tume na usimamizi
wa chaguzi kwa lengo la kuboresha na kuimarisha demokrasia nchini
Tanzania. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaisihi Tume ya
Uchaguzi bila kujali madhaifu katika uwasilishaji, kufanyia kazi
changamoto zinazoibuliwa na wadau kwa lengo la kujenga Jamii yenye Haki
na Usawa.
Imetolewa na;
Naemy Sillayo (Wakili)
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
No comments:
Post a Comment