Wednesday, March 7, 2018

Rais Magufuli atuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Mjini


“Kwa masikitiko nimepokea taarifa ya kifo cha Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma Dkt. Walid Amani Kaburu kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 07 Machi, 2018 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Dkt. Walid Amani Kaburu atakumbukwa kwa mchango wake alipokuwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM, na alipokuwa Mbunge wa Kigoma Mjini na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

Natoa pole kwa familia yake, wana CCM wote, wananchi wa Kigoma, ndugu jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu”

Hii ni sehemu ya salamu za rambirambi alizotuma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga kufuatia kifo cha Dkt. Walid Amani Kaburu.

Pamoja na salamu hizo Mhe. Rais Magufuli ameiombea familia ya Marehemu na wote walioguswa na msiba huu kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi na amemuombea Marehemu apumzike mahali pema peponi, Amina.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
07 Machi, 2018

No comments:

Post a Comment