Friday, March 23, 2018

TIRA yazifutia leseni kampuni nne za udalali na ushauri

Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima nchini (TIRA) imefuta leseni za kampuni za udalali na ushauri wa Bima kutokana na kukiuka taratibu za uendeshaji wa biashara za bima.

Akizungumza na wanahabari jana  jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Bima wa TIRA, Dkt. Baghayo Saqware amesema kampuni hizo zimekuwa zikichafua taswira ya biashara ya bima pamoja na kutishia soko la bima nchini.

“Makampuni haya yameshindwa kuwasilisha tozo za bima kwa makampuni ya bima, hivyo kuwanyima wateja wa bima haki ya kunufaika na fidia ambazo zingetolewa na makampuni endapo fedha hizi zingewasilishwa,” amesema.

Dkt. Saqware amezitaja kampuni hizo ikiwemo Kampuni ya Udalali wa Bima ya Hans, Kampuni ya Endeavour, Leegend of East Africa na Kampuni ya Swift.

Amesema TIRA inaendelea kushirikiana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ili kuzichukulia hatua za kisheria baadhi ya kampuni zisizowasilisha ada za bima kwa kampuni za bima husika baada ya kupokea kutoka kwa wateja pamoja na kukwepa ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa na mamlaka hiyo.
Amezitaja kampuni hizo kuwa ni, Kampuni ya Udalali wa Bima ya Pacific na Kampuni ya Core.

No comments:

Post a Comment