Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali
Mstaafu Salum Kijuu kufuatia watu 11 kupoteza maisha katika ajali ya
gari iliyotokea katika Kijiji cha Nyangozi, Wilaya ya Biharamulo Mkoani
Kagera.
Ajali
hii imetokea jana tarehe 14 Januari, 2018 majira ya saa 11 jioni baada
ya basi dogo la abiria aina ya Nissan Caravan lililokuwa likitoka
Kakonko Mkoani Kigoma kuelekea Kahama Mkoani Shinyanga kuligonga ubavuni
lori la mizigo kisha kugongana uso kwa uso na lori jingine na
kusababisha vifo vya watu 11 na wengine 6 kujeruhiwa.
Mhe.
Rais Magufuli amepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za vifo
vya Watanzania hao na amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali
Mstaafu Salum Kijuu kumfikishia pole kwa familia za Marehemu wote,
ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo.
“Nimehuzunishwa
na kusikitishwa sana na vifo hivi, nawapa pole wafiwa wote, ninawaombea
marehemu wapumzike mahali pema na majeruhi wapone haraka ili waweze
kuungana na familia zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wa barabara hasa madereva
kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na ameviagiza
vyombo vinavyohusika kuongeza jitihada za kukabiliana na ajali za
barabarani ili kuokoa maisha ya watu na mali zinazopotea kutokana na
ajali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Januari, 2018
No comments:
Post a Comment