Serikali
imesema haijazuia matumizi ya fedha za kigeni nchini bali imechukua
hatua ya kudhibiti matumizi ya fedha hizo kulinda thamani ya shilingi ya
Tanzania.
Kauli
hiyo imetolewa leo Januari 15, 2018 na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk Ashatu Kijaji alipokutana na wawakilishi wa wafanyabiashara
mkoani Arusha kujadiliana mambo mbalimbali kwa ajili ya kukuza sekta ya
biashara nchini.
Amesema
sheria haijazuia matumizi ya fedha hizo nchini, inasisitiza kuwa watu
wanapaswa kutambua kuwa sarafu ndiyo fedha halali kwa malipo ndani ya
nchi.
“Tatizo
kubwa tunalokumbana nalo ni uhuru ulioachiwa unaosababisha kushuka kwa
thamani ya shilingi yetu. Kila mmoja anaweza kutumia fedha za kigeni,
pia watumiaji wa fedha za kigeni hawafuati thamani ya fedha iliyoko
sokoni. Kila mmoja anakuwa na kiwango tofauti cha thamani ya kubadili
fedha,” amesema Dk Kijaji.
Amebainisha
kuwa ili kuondoa changamoto hizo Serikali imeamua kurekebisha sheria ya
matumizi ya fedha za kigeni na sheria ya Benki Kuu (BoT) ambayo
inazitaka bei zote nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania.
Amesema
bei hizo zinajumuisha kodi za nyumba za kuishi na ofisi, bei za ardhi,
gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya
kielektroniki.
“Bei
ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja ambao sio wakazi
zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza
kufanyika kwa fedha za kigeni,” amesema na kuongeza,
“Hata hivyo kama mlengwa akitaka kulipa kwa shilingi ya Tanzania asilazimishwe kulipa kwa fedha za kigeni.”
Amezitaka vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaokiuka maagizo hayo yaliyotolewa na Serikali.
No comments:
Post a Comment