Jeshi la Polisi limesema msako dhidi ya Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Ami Lukule, ambaye anatuhumiwa kwa mauaji ya mkewe, kichanga chake na shemejiye wa kike, unaendelea vizuri na wanaamini kuwa watamtia mbaroni wakati wowote.
Lukule anadaiwa kutekeleza mauaji hayo kwa kutumia jembe la kulimia Jumatano iliyopita, katika eneo la Masota Darajani, Goba jijini Dar es Salaam. Waliofariki kutokana na tukio hilo ni Pendo Lukule, kichanga chake cha umri wa miezi minne, Joshua na shemeji wa kike wa mtuhumiwa ambaye ni ndugu wa mkewe, Magreth Samwel.
Inadaiwa kuwa Lukule alikimbilia kusikojulikana mara tu baada ya kufanikisha mauaji hayo, huku akiacha ujumbe unaowataka polisi kutohangaika kwa sababu ni yeye aliyetekeleza mauaji kutokana na kitendo cha mkewe kutokuwa mwaminifu na kwamba hata mtoto aliyemuua siyo wa kwake bali mkewe amezaa na watu wengine.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Benedict Kitalika, amesema kuwa hadi sasa, wanaendelea vizuri na msako dhidi ya mtuhumiwa kwa sababu wameshapata taarifa muhimu za kumtia mbaroni wakati wowote kuanzia sasa.
“Tumeshapokea taarifa na tunaamini zitatusaidia kumpata… yupo hapa nchini. Jeshi letu lipo vizuri, tutamkamata na kumchukulia hatua dhidi ya mauaji aliyoyafanya,” amesema Kitalika.
Katika hatua nyingine, taarifa zilidai jana kuwa miili ya marehemu inatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Kinondoni.
No comments:
Post a Comment