Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina amekamata kilo 65600 za
samaki wachanga aina ya Sangara waliokaushwa kwa chumvi wenye thamani ya
shilingi milioni mia tatu katika Kisiwa cha Lubili wilayani Muleba kwenye Mkoa
wa Kagera baada ya wamiliki wa samaki hao kukimbia.
Akizungumza leo na Waandishi wa Habari katika Ofisi ya Kitengo cha Doria
na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera, Mpina amesema tukio la
kukamatwa kwa samaki hao lilifanikiwa baada kupata taarifa kutoka kwa raia
mwema ambapo aliagiza mamlaka za Wilaya ya Muleba kufuatilia kwa karibu
hatimaye kuwakuta samaki hao wakiwa wameanikwa chini katika kisiwa hicho.Waziri Mpina amesema Sheria ya Uvuvi namba 22 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 kifungu cha 90(1) inataka samaki wanaovuliwa waandaliwe katika mazingira yanayokidhi vigezo vya usalama kwa mlaji na kwamba ni kosa kisheria kuwavua au kuchakata samaki aina ya Sangara walio chini ya sentimeta 50 kwa kuwa ni wachanga na sentimita 25 kwa Samaki aina ya Sato. Pia sentimita 85 kwa Sangara kwa kuwa ni wazazi wanaotakiwa kundelea kuzaa.
Waziri ameongeza kuwa Sheria hiyo imetoa mamlaka kwa watendaji wa
Serikali kutaifisha mali zote zilitumika katika uvuvi haramu kupitia kifungu
cha 37(a) (ii) na (iii) pamoja na Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu
namba 29 ya mwaka 1994.
Aidha Waziri Mpina ameagiza watendaji kufuata taratibu zote za kisheria
ili samaki hao wauzwe kwa njia ya mnada na mapato hayo yaingie Serikalini mara
moja.Aidha aliwaonya wafanyabiashara na wavuvi kuachana na uvuvi haramu kwa
kuwa ni kuhujumu raslimali za taifa ambazo zingetumika kwa kizazi cha sasa na
baadaye.
No comments:
Post a Comment