Monday, February 12, 2018

ARDHI YASABABISHA MGOGORO KATI YA FAMILIA NA SERIKALI MJINI GEITA

Baadhi ya eneo ambalo linalalamikiwa na Sizya Mashirungu kuvamiwa na kujengwa shule na serikali kinyume na makubaliano kati yake halmashauri ya Mji wa Geita. 

Mwenyekiti wa mtaa Shinde Bw Makoye Mumilambo akizungumza juu ya malalamiko ambayo yametolewa na Bw,Sizya Mashirungu juu ya kutaka kutahifishwa eneo la familia na serikali ya mtaa huo. 
Eneo linalolalamikiwa likiwa tayari limeshaanza kuchimbwa Msingi kwaajili ya ujenzi wa shule ya Msingi ya Shinde. 


Na Joel Maduka ,Geita.

Familia ya Bw Mlelemi Mashirungu inayoishi mtaa wa Mkolani Kata ya Nyankumbu wilayani Geita imeilalamikia serikali kwa kuanzisha ujenzi wa shule ya msingi Shinde kwenye shamba la ukoo huo lenye ukubwa wa ekari 20 bila makubaliano na serikali ya Halmashauri ya mji wa Geita .

Msimamizi wa eneo hilo Bw Sizya Mashirungu amesema eneo la ujenzi wa shule hiyo lilitengwa na serikali ya kijiji kabla ya kubadilishwa na kuwa mitaa lakini ameshangazwa na kitendo cha serikali kuanzisha ujenzi katika eneo lake bila makubaliano.

Bw Mashirungu alisema eneo hilo limeanza kumilikiwa na ukoo tangu mwaka 1991 baada ya Baba yao mzazi kufariki na kwamba limekuwa likitumika katika shughuli za kilimo.

“Anayezungumza kuwa hii ni hifadhi akuna ofisi yoyote ambayo ilishawai kufika kuweka pingamizi juu ya eneo hili na mshangaa mwenyekiti ambaye anangangania kuwa eneo hili ni la hifadhi yani huu ni utapeli kabisa na mimi sitakubaliana na maamuzi ambayo yanataka kuchukuliwa na serikali juu ya matumizi ya eneo hili”Alisema Mlelemi.

Aidha kutokana na malalamiko kumuelekea Mwenyekiti wa mtaa huo Bw Makoye Mumilambo kutaka kuhujumu eneo la ukoo huo, Kwa upande wake amesema eneo hilo lipo ndani ya hifadhi ya halmashauri ya mji wa Geita na kwamba watu wamekuwa wakimiliki maeneo hayo kinyume na utaratibu tangu mwaka 1978 na kwamba hata yeye ni mvamizi kutokana na miti iliyokuwepo kukatwa hivyo serikali imeamua kubadili matumizi ya eneo hilo.

Diwani wa kata hiyo Bw Machael Kapaya alisema madai ya Bw Masirungu sio ya kweli kwa kuwa miradi inayoanzishwa michakato huanzia kwenye ngazi ya chini ambayo ni wananchi ambao wanapendekeza mahitaji yao na kwambe yeye ni moja kati ya viongozi wa mitaa na anajua utaratibu.

“Huyu ni kiongozi kabisa wa mtaa na anajua taratibu zote ambazo zinafanyika kuibua miradi kwenye mitaa na wakati tunapendekeza eneo hilo alikuwepo kwenye kikao cha kamati ya maendeleo ya kata na tulikwisha mwambia kama anamadai alete vielelezo ambavyo vinathibitisha kuwa ni eneo lake lakini hadi sasa ajaleta na tukimwambia aje kwa mkurugenzi anachenga chenga”Alisema Kapaya.

Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Geita Mhandisi Modesti Apolinary alisema eneo linalotumika katika ujenzi wa shule ni eneo la hifadhi na kwamba hakuna mtu anayeruhusiwa kumiliki eneo lililo ndani ya hifadhi ya serikali.

No comments:

Post a Comment