Mahakama
ya Rufaa imemwondolea Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) mamlaka ya kuzuia
dhamana ya mshtakiwa bila hata kulazimika kutoa sababu, baada ya
kubatilisha kifungu cha 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya
Jinai, kinachompa mamlaka hayo.
Kifungu
hicho kinampa DPP mamlaka ya kuizuia Mahakama au ofisa wa polisi kutoa
dhamana kwa mshtakiwa au mtuhumiwa baada ya kuwasilisha hati ya
maandishi, kwa maelezo kuwa usalama au masilahi ya Jamhuri yataathirika.
Mahakama
hiyo katika hukumu ya rufaa ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya
mwanaharakati wa haki za binadamu, Jeremia Mtobesya imesema kifungu
hicho ni kinyume cha Katiba na ni batili.
Hukumu iliyotolewa na jopo la majaji watano wa Mahakama ya Rufaa imekubaliana na ya awali iliyotolewa na Mahakama Kuu.
Majaji
waliosikiliza na kutoa hukumu ya rufaa hiyo ni Bernard Luanda (kiongozi
wa jopo), Kipenka Mussa, Bethuel Mmila, Stellah Mugasha na Jacob
Mwambegele.
Hukumu
hiyo ilisomwa Ijumaa iliyopita na Msajili wa Mahakama ya Rufaa, John
Kahyoza aliyesema kifungu hicho kwa jinsi kilivyo, Mahakama au ofisa wa
Polisi anakuwa hana uchaguzi zaidi ya kumnyima dhamana mshtakiwa au
mtuhumiwa.
Alisema
kifungu hicho hakikidhi matakwa ya kisheria kwa kuwa haipaswi kuwa ya
maelezo ya jumla na kinaweza kutoa mwanya wa matumizi mabaya ya mamlaka
kwa DPP.
Baada
ya kufanya rejea ya sheria na uamuzi wa kesi kadhaa za ndani na nje ya
nchi, Kahyoza alisema Mahakama imejiridhisha kuwa masharti ya kifungu
hicho ni kinyume cha Katiba na hivyo ni batili.
Akizungumzia jana kuhusu hukumu hiyo, Mtobesya alisema Mahakama imeitoa kwa misingi ya kikatiba.
“Katiba
ndivyo inavyoelekeza kuwa mtu yeyote ana haki ya kusikilizwa na kila
mtu ana haki ya kuwa huru. Sasa iwapo hizo haki zinaweza zikaondolewa,
kuna utaratibu ambao unawekwa kisheria,” alisema.
Mtobesya
alisema, “Kwenye ngazi zote, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa
zimeangalia na kujiridhisha kwamba sawa hizo haki zinaweza kuwa si
absolute (kamilifu) lakini je misingi ya kunyimwa hizo haki imefuatwa?”
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali alikata rufaa akipinga hukumu ya Mahakama Kuu ya
Desemba 22,2015 iliyotolewa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji
Kiongozi, wakati huo, Shaban Lila. Majaji wengine walikuwa Sekieti
Kihiyo na Profesa Eudes Ruhangisa. Katika shauri la msingi la madai
namba 29 la mwaka 2015, Mtobesya ambaye ni wakili wa kujitegemea alidai
kifungu hicho kwa jinsi kilivyo kinamnyima mshtakiwa aliye mahakamani au
mtuhumiwa aliye polisi haki ya kusikilizwa.
Katika
hoja za maandishi, alidai kila kesi inaangaliwa kwa mazingira yake na
kwamba, kitendo cha DPP kuzuia tu dhamana kwa madai kwamba itaathiri
masilahi ya umma bila kutoa sababu kinamnyima haki mhusika.
Alidai
maelezo hayo tu ya kuathiri masilahi ya umma hayatoshi bali anapaswa
kwenda mbali zaidi na kutoa sababu na kisha mshtakiwa au mtuhumiwa naye
apewe nafasi ya kusikilizwa ndipo Mahakama ipime na kutoa uamuzi kwa
sababu hizo.
Mahakama
Kuu katika hukumu yake ilikubaliana na hoja za Mtobesya, ikisema
kifungu hicho kinamnyima mtu haki ya kusikilizwa na ni kinyume cha Ibara
ya 13 (6) ya Katiba ya nchi.
Mahakama ilisema kifungu hicho kinaenda kinyume cha misingi ya kidemokrasia.
Hukumu
hiyo katika kesi ya jinai, DPP na mshtakiwa wote wanakuwa na haki sawa
lakini kifungu hicho kinaupa upande mmoja mamlaka zaidi na kuufanya
mwingine kuwa dhaifu, hivyo kutokuwa na usawa.
Mahakama Kuu ilisema kifungu hicho kinaondoa mamlaka ya Mahakama kuwasikiliza wadaiwa.
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali hakukubaliana na uamuzi huo, hivyo alikata rufaa
Mahakama ya Rufaa akiwasilisha hoja tano za kuipinga. Wakati wa
usikilizwaji aliondoa hoja tatu zikabaki mbili.
Pamoja
na mambo mengine, AG aliipinga hukumu hiyo akidai kifungu hicho kiko
sawa kwa kuwa kuna ibara za Katiba ambazo zinakifanya kiwe hivyo
kilivyo, sawa na ibara ya 30 (2) (a) ya Katiba.
Mtobesya
kupitia kwa wakili wake Mpale Mpoki alipinga hoja zilizotolewa na AG
kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Timon akidai kifungu hicho kwa
namna kilivyo hakimpi fursa mshtakiwa kusikilizwa kabla ya kuzuiwa
dhamana kwa hati ya DPP.
Wakili
Mpoki alidai kifungu hicho kinakiuka ibara ya 13 (6) ya Katiba ya nchi,
huku akiungwa mkono na Profesa Gamaliel Mgongo Fimbo aliyealikwa na
Mahakama kutoa maoni ya kitaalamu.
Profesa
Mgongo Fimbo pamoja na mambo mengine alisema kifungu kinachomzuia
mshtakiwa kusikilizwa maombi yake ya dhamana au kupinga hati ya DPP,
hakiweki usawa wa usikilizwaji, hivyo kinakiuka ibara ya 13 (6) (a) ya
Katiba.
No comments:
Post a Comment