Ndege
mbili; moja aina ya Bombardier na nyingine kubwa Boeing 787 yenye uwezo
wa kubeba abiria 262 zilizonunuliwa na serikali, zinatarajiwa kuwasili
nchini Julai mwaka huu.
Serikali
imenunua ndege hizo ikiwa ni mkakati wa kuimarisha Shirika la Ndege
(ATCL) ili limudu ushindani kwenye biashara ya kusafirisha abiria na
kujiendesha kwa faida.
Akiwasilisha
taarifa ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa
kipindi cha Januari 2017 hadi, jana, mjini hapa, Mwenyekiti wa kamati
hiyo, Prof. Norman Sigalla, alisema wamejulishwa kuwa pamoja na ndege
mbili mpya aina ya Dash 8 Q400, Julai serikali inategemea kupokea ndege
zingine mbili ambapo moja ni Dash 8 Q400 na nyingine aina ya Boeing 787
yenye uwezo wa kubeba abiria 262.
Alisema
kwa sasa ATCL ina ndege tatu zinazofanya safari ndani na nje ya nchi,
lakini akasisitiza kuwa biashara ya ndege inahitaji mikakati mikubwa ya
kibiashara kuweza kuingia katika soko la ushindani.
"ATCL
iangaliwe kama kampuni ya kibiashara na siyo kutoa huduma na ijitangaze
kwenye vyombo rasmi vya kimataifa ambavyo huonyesha safari za ndege
duniani," alisema.
"Kampuni
ijipange kuingia katika soko kwa kujitangaza kwenye vyombo vya habari,
majarida, vipeperushi, kujali wateja, kuwa na bei nafuu ili kuhakikisha
abiria wengi wanatumia ndege hizo."
Prof.
Sigalla pia alisema Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) inashauriwa
kuhakikisha viwanja vya ndege visivyokuwa na hati vinapimwa kisha
kupatiwa hati miliki.
Alisema viwanja hivyo pia vinapaswa kuwekewa uzio kuepusha uvamizi wa maeneo jambo ambalo huleta migogoro na wananchi.
"Ili
kuongeza udhibiti na ulinzi katika viwanja vya ndege vilivyopo mipakani
kama vile Mtwara, Kigoma na Kagera kuepusha viwanja hivyo kupitishwa
biashara haramu," alisema.
No comments:
Post a Comment