Wednesday, February 7, 2018

PROF. KABUDI: “HAKUNA MGONGANO WA KIMAMLAKA KATIKA KATIBA YA TANZANIA NA ZANZIBAR”

Serikali imesema Kikatiba hakuna mgongano wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar unaosababisha ongezeko kubwa la kero za Muungano na mgongano wa kimamlaka baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.



Hayo yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi bungeni jana mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Wingi Mhe. Juma Kombo lililohusu mgongano wa Katiba hizo.




Prof Kabudi alisema kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka utaratibu mahususi wa kushughulikia tafsiri
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na utekelezaji wake inayobishaniwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.



“Hadi sasa hakuna upande wowote baina ya Serikali hizi mbili ambao unatafsiri tofauti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano au utekelezaji wake”



“Hivyo kwa kuzingatia kuwa hakuna mgongano wa Katiba kati ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali haina sababu ya kuleta mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ili kuondoa changamoto hiyo ambayo haipo.” alifafanua Prof Kabudi.



Akizunguzmzia kuhusu mgongano wa kimamlaka Prof. Kabudi alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anamamlaka yote katika masuala yanayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



Aidha, akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Mjini Mary Chandanda kuhusu upandishwaji vyeo kwa Mahakimu na Watumishi wa Mahakama, Prof Kabudi alisema kuwa suala la kupandisha vyeo watumishi wenye sifa stahiki ni wajibu endelevu kwa Serikali.



“Mahakama ya Tanzania imekuwa ikichukua hatua kuwapandisha Mahakimu na Watumishi wa ngazi mbalimbali vyeo kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kisheria ikiwa ni pamoja na muda wa utumishi kazini, utendaji kazi, weledi na maadili pamoja na upatikanaj wa vibali kutoka Idara Kuu ya Utumishi,” alisema Prof Kabudi.



Hata hivyo, Prof. Kabudi alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2012/2013 jumla ya Mahakimu na Wasaidizi wa Sheria wa Majaji 52 walipandishwa vyeo, mwaka 2013/2014 jumla ya watumishi 200 walipandishwa vyeo, mwaka 2014/2015 Mahakimu na Wasaidizi wa Sheria wa Majaji 22 na watumishi 686 walipandishwa vyeo na mwaka 2015/2016 Mahakimu na Wasaidizi wa Sheria 59 na watumishi 447 walipandishwa vyeo.

No comments:

Post a Comment