Jeshi
la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria
zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu
na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada
hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa
ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.
Aidha
Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio
makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa
kushirikiana na wananchi kuhakikisha mkoa wetu unakua mahala salama.
Hata hivyo kumekuwa na matukio kama ifuatavyo:-
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WATATU WAKIWA NA NYARA ZA SERIKALI.
Mnamo
tarehe 05 Februari, 2018 majira ya saa 19:45 usiku huko maeneo ya
Mwanjelwa, Kata ya Ruanda, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya, Jeshi la
Polisi Mkoa wa Mbeya likiwa katika majukumu yake ya kuhakikisha usalama
wa raia na mali zao, limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na
nyara za Serikali ambazo ni vipande vinne vya meno ya Tembo.
Watuhumiwa
waliokamatwa wamefahamika kwa majina ya 1. KENEDY LUPEMBE SIMSOKWE [43]
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha SAUT – Tawi la Mbeya na Mkazi wa Iyela 2.
MATHEW ELIKANA MWANJALA [42] Mpiga picha na Mkazi wa Iyela na 3. SHABAN
MKWICHE [24] Mkazi wa Iyunga.
Aidha
baada ya kukamatwa na kupekuliwa, watuhumiwa walikutwa na nyara hizo
[Vipande vinne vya Meno ya Tembo] ambavyo vina uzito wa kilogram 5 na
thamani ya Tshs 33,000,000/=.
Taratibu za kisheria zinafanyika ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani kwa hatua zaidi.
WITO:
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA
anatoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuwa na tamaa ya kujipatia utajiri
wa haraka kwa kutumia njia za mkato zisizo halali, badala yake wafanye
kazi halali ili kupata kipato halali. Aidha Kamanda MPINGA anatoa rai
kwa yeyote mwenye taarifa juu ya mtu/ watu au kikundi /mtandao wa watu
wengine wanaojihusisha na matukio ya ujangili wazitoe katika mamlaka
husika ili hatua za kisheria dhidi yao zichukuliwe mara moja.
Imesainiwa na:
[MOHAMMED R. MPINGA – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
No comments:
Post a Comment