Thursday, February 15, 2018

Maofisa 18 Watimuliwa Uhamiaji

Idara  ya Uhamiaji imewatangaza maofisa 18 wa ngazi tofauti kutohusika ama kutambua huduma yoyote itakayotolewa nao kwa sababu si wafanyakazi tena.

Hatua hiyo imetokana na idara hiyo hivi karibuni kupokea malalamiko mengi kupitia kampuni na taasisi mbalimbali kuwa kuna watu wanapita kwenye ofisi wakijitambulisha kuwa maofisa kutoka uhamiaji.

Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda,  jana alisema kutokana na hali hiyo, wameamua kuwatangaza watu hao ambao baadhi walisimamishwa kwa makosa ya rushwa na utovu wa nidhamu.

Mtanda alisema idara ya Uhamiaji iliwasimamisha kazi watu hao mwaka 2016/17 na kwamba wengine waliacha kazi wenyewe.

Alisema wameamua kufanya hivyo ili chochote kitakachojitokeza dhidi yao, idara haitahusika.

“Tumeamua kuwatangaza kwa sababu hivi karibuni tumepokea malalamiko mengi kupitia kampuni na taasisi mbalimbali kuwa kuna watu wanapita kwenye ofisi hizo wakijitambulisha kuwa maofisa kutoka uhamiaji.

“Hawa tuliowatangaza leo (jana) kuwa sio wafanyakazi tena wa Idara ya Uhamiaji lengo ni ili jambo lolote likitokea huko nje dhidi yao itambulike si watumishi wetu tena,” alisema.

Mtanda alisema orodha hiyo ambayo imeambatanishwa na picha za watu hao ni kwa lengo la umma kuwatambua kuwa si wafanyakazi wa idara hiyo tena.

Katika tangazo lililotolewa juzi na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, idara hiyo haitahusika au kutambua huduma yoyote itakayotolewa na watajwa kwenye picha.

Watu hao ni Thobias Lyewe, Julieth Mrema, Nina Muga, Loveness Wilson, Wilbard Ompapson, Salama Dilunga, Philbert Chaula, Mkombozi Chodri na Alfred Mrema.

Wengine ni Imaculata Mwakatika, Ramadhani Ally, Ritha Maganga, Jovin Mkuchu, Veronika Max, Angela Mwambwiga, Peter Bally, Elizabeth Kibinga na Lucy Munyanga.

No comments:

Post a Comment