Friday, February 9, 2018

Bashe awahenyesha mawaziri watano, wakutana kwa dharura

Mawaziri watano jana walilazimika kufanya kikao cha dharura bungeni baada ya uongozi wa Bunge kuagiza serikali itoe majibu kutokana na hoja ya Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe.


Mawaziri waliokutana kutokana na hoja hiyo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo; Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Waziri wa Nishati,Dk. Medard Kalemani na naibu mawaziri wa fedha, Dk. Ashatu Kijaji na wa maji, Jumaa Awesso.

Mbunge huyo aliwashtaki mawaziri kwenye chombo hicho cha kutunga sheria akieleza kuwa wamekuwa chanzo cha mateso na mahangaiko kwa wananchi wa Nzega.

Huku akitumia Kanuni ya 47 kuliomba Bunge liahirishe shughuli zake za jana na kujadili jambo la dharura, Bashe aliwataja hadharani Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Tamisemi, Selemani Jafo, ambao alidai wamesababisha wananchi wa jimbo lake kukosa maji kwa siku ya 13 mfululilo hadi kufikia jana.

Alisema huduma hiyo haiko jimboni kwake kwa kipindi hicho cha wiki mbili kutokana na mamlaka ya maji kukatiwa umeme kutokana na serikali kutolipa malimbikizo ya madeni kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Mbunge huyo alisema amekuwa akiwasiliana na serikali lakini hakuna kinachoendelea na wahusika wamekaa kimya ilhali wananchi wa jimbo lake hilo wanapata taabu.

“Ndugu zangu wabunge na hasa wabunge wa CCM, naombeni mniunge mkono katika jambo hili. Nzega ni siku ya 13 sasa hatuna maji, wanawake wanateseka bila maji na kunilazimu ninunue maji kwa ajili ya hospitali,” alisema Bashe aliyeonekana kuzungumza kwa hisia kali.

Alibainisha kuwa yuko tayari kwa jambo lolote kwa kuwa ni wananchi wake wanaoumizwa na serikali kwa kukatiwa maji katika kosa ambalo serikali ndiyo mhusika mkuu wa deni hilo.

Alisema wananchi wake wanapata mateso lakini serikali haijawahi kupeleka majibu ya aina yoyote kuhusu mateso hayo na bado inaonekana kutojali licha ya Bunge kutaka mawaziri wakutane naye kujadiliana.

"Waheshimiwa wabunge, naomba tusaidiane katika kumsaidia Rais wetu, hali ni mbaya. Wapendwa leo ni Nzega, lakini itakuwa kesho kwa mwingine, lolote litalotokea huko litakuwa juu ya mawaziri hao,” alisema Bashe na kutoa hoja.

Kutokana na hoja hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliyekuwa anaongoza kikao cha jana, alisimama na kueleza ukubwa wa tatizo la maji kuwa ni la nchi nzima, hivyo halitakiwi kuupuzwa na akaomba kuwatendea haki wananchi katika maeneo yote.

Kwa uzito huo, Chenge alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, kueleza hatua ambazo zimechukuliwa na serikali kutatua changamoto hiyo.

Waziri huyo aliagiza mawaziri wanaohusika na maji, nishati na fedha kukutana kwa dharura kwenye moja ya kumbi za Bunge mara moja pamoja na Bashe baada ya kuahirishwa kwa shughuli za chombo hicho jana mchana.

Kutokana na majibu hayo, wabunge wengi walisimama na kuomba miongozi huku Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), akieleza kuwa tatizo la maji kuwa ni kubwa na hata katika wilaya yake ambako watumishi walikula fedha za mradi wa maji lakini wakahamishwa na kuacha mradi ukiwa haujakamilika.

Nje ya Bunge, Bashe alisema kuwa kikao baina yake na mawaziri hao kilifanyika kwa nusu saa kwenye moja ya kumbi ndogo zilizoko ndani ya jengo la Ukumbi wa Bunge na akabainisha kuwa katika kikao hicho waliazimia serikali iji-commit' kulipa deni la umeme na mamlaka ya maji irudishiwe huduma ya umeme haraka.

No comments:

Post a Comment