Wednesday, September 6, 2017

MAFUTA YA TAA YASHUKA, PETROL, DIZELI BEI JUU.

Mamlaka  ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei mpya ya bidhaa za mafuta ya petroli nchini, ambapo kuanzia leo bei za rejareja za bidhaa hizo zimepanda kwa Sh 10 kwa lita, ikilinganishwa na bei iliyopita huku bei ya mafuta ya taa ikishuka.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Godwin Samwel, kuanzia Septemba mwaka huu, bei za rejareja za petroli na dizeli zimeongezeka
kwa Sh 10 kwa lita sawa na ongezeko la asilimia 0.53 na Sh 57 kwa lita sawa na asilimia 3.10.
Hata hivyo, bei ya mafuta ya taa imepungua kwa Sh 19 kwa lita sawa na asilimia 1.04. 
Aidha, ilisema kuwa kwa kulinganisha na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli na dizeli, nazo zimeongezeka kwa Sh 10.41 kwa lita sawa na asilimia 0.56 na Sh 56.74 kwa lita sawa na asilimia 3.30.
Alisema kwa upande wa mafuta ya taa, bei ya bidhaa hiyo imepungua kwa Sh 10.01 kwa lita sawa na asilimia 1.11. 
Alifafanua kuwa ongezeko la bei za petroli na dizeli kwenye soko la ndani, limetokana na ongezeko la bei za mafuta hayo katika soko la dunia na ongezeko la gharama za usafirishaji wa mafuta hayo (BPS premiums).
Kupungua kwa bei ya mafuta ya taa kunatokana na kupungua kwa gharama za usafirishaji wa mafuta hayo, ijapokuwa bei ya mafuta hayo imeongezeka katika soko la dunia. 
Alieleza kuwa kutokana na mabadiliko hayo mapya ya bei za bidhaa za mafuta, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote katika mkoa wa Tanga, nazo zimebadilika, ikilinganishwa na toleo lililopita la tarehe Agosti 2, mwaka huu.
Katika mkoa huo, kuanzia Septemba mwaka huu, bei za rejareja za petroli zimeshuka kwa Sh 13 kwa lita sawa na asilimia 0.65 wakati bei za Dizeli na Mafuta ya Taa zimeongezeka kwa Sh 14 kwa lita sawa na asilimia 0.78 na Sh 106 kwa lita sawa na asilimia 6.21.
Aidha, bei za jumla za petroli zimeshuka kwa Sh12.98 kwa lita sawa na asilimia 0.69 wakati bei za dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa Sh 14.47 kwa lita sawa na asilimia 0.83 na Sh 105.88 kwa lita sawa na asilimia 6.65).
Samwel alifafanua kuwa kupanda na kushuka kwa bei za mafuta mkoani Tanga, kunatokana na mabadiliko ya bei za mafuta hayo katika soko la dunia na ongezeko la gharama za usafirishaji wa mafuta hayo.
Alisema vituo vyote vya mafuta, vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango, yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta.

No comments:

Post a Comment