Mahakama ya Juu imefuta matokeo ya urais yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta kuwa madarakani kwa muhula wa pili.
Mgombea
wa Muungano wa Nasa, Raila Odinga alifungua kesi mahakamani kupinga
matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Agosti 8, akisema ulitawaliwa na
udanganyifu ikiwemo kuchezewa mitambo ya kujumlishia matokeo.
Katika
uamuzi wake, Mahakama imesema uchaguzi huo ulikuwa na dosari nyingi,
hivyo kukiuka misingi ya uchaguzi huru na wa haki kama ilivyoelekezwa
katika Katiba ya nchi hiyo.
Hii
ni mara ya kwanza katika historia ya Taifa hilo kwa Mahakama ya Juu
kufuta matokeo ya uchaguzi na inaweka rekodi mpya katika historia ya
uchaguzi barani Afrika ndani ya mfumo wa vyama vingi.
Katika
uchaguzi uliopita, Odinga alienda mahakamani kupinga matokeo lakini
Mahakama hiyo ilitupilia mbali hoja zake na kuridhia matokeo yaliyompa
ushindi Rais Kenyatta.
Katika
uchaguzi wa Agosti 8, Kenyatta alitangazwa mshindi kwa kupata kura
8,203,290 sawa na asilimia 54.27, huku mpinzani wake Odinga akipata kura
6,762,224 sawa na asilimia 44.74.
Kwa
uamuzi uliotolewa na mahakama, uchaguzi mwingine unapaswa kufanyika
katika kipindi cha siku 60. Iwapo ushindi wa Kenyatta ungeidhinishwa
angepaswa kuapishwa Septemba 12.
Kumekuwa
na shamrashamra katika mitaa mbalimbali ya Nairobi na Mombasa
kushangilia uamuzi huo, huku Odinga akiwa na wanasiasa wenzake
wamepongeza wakisema watatoa taarifa zaidi baadaye.
No comments:
Post a Comment