Mwanafunzi
Wilson Tarimo, aliyenusurika katika ajali ya basi iliyoua wanafunzi
32 wa Shule ya Msingi Lucky Vincent ni miongoni mwa mashahidi 15 wa
upande wa Jamhuri kwenye kesi inayomkabili mmiliki wa shule hiyo,
Innocent Moshi.
Moshi anakabiliwa na tuhuma za makosa ya usalama barabarani ikiwamo kusafirisha wanafunzi bila kuwa na vibali muhimu.
Katika
kesi hiyo namba 78 ya mwaka huu, Moshi pamoja na Mwalimu Mkuu Msaidizi
wa shule hiyo, Longino Nkana, jana walisomewa hoja za awali katika
Mahakama ya Wilaya ya Arumeru.
Mbele
ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Desderi Kamugisha, Wakili wa
Jamhuri, Khalili Nuda, alidai Jamhuri inatarajia kuwa na mashahidi 15
katika kesi hiyo, pamoja na vielelezo 12.
Mashahidi
wengine ni Ofisa Kazi Mfawidhi wa Idara ya Kazi Mkoa wa Arusha, Wilfred
Mdemi, Mohamed Matumula kutoka Kampuni ya Bima ya Zanzibar Insurance,
Songoyi Jilala (askari wa usalama barabarani Arusha), Koplo Hamad
(Karatu), Inspekta Shukrani (askari wa usalama barabarani Arusha), Koplo
Saada (trafiki Arusha) na E.4312 PC Mugobe (trafiki Arusha).
Wengine
ni Mkuu wa Polisi wa Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha (RTO), Nuru
Suleiman, G 4130 PC Mwita (askari wa usalama barabarani Karatu), Ignatus
Paul(Karatu), Leonidas Gerald (Morombo) na Hamis Omary mkazi wa
Sombetini.
Wakili
Nuda alitaja vielelezo hivyo kuwa ni kadi ya gari namba T 871 BYS,
mkataba wa ununuzi wa gari, Barua ya RTO kwenda Sumatra ya Mei 8 mwaka
huu, barua ya RTO kwenda Zanzibar Insurance ya Mei 8, mwaka huu na
taarifa ya Zanzibar Insurance ya Mei 9 mwaka huu.
Vingine
ni taarifa ya Sumatra ya Mei 9 mwaka huu, taarifa ya idara ya kazi,
taarifa ya ukaguzi wa gari, ramani ya eneo la tukio, maelezo ya
mshitakiwa wa kwanza na maelezo ya mshitakiwa wa pili.
Wakili huyo aliiomba mahakama hiyo kutoa wito kwa mashahidi hao.
Akiwasomea
hoja hizo za awali, Wakili Nuda alidai katika shitaka la kwanza
linalomkabili Moshi, ni kufanya biashara ya usafirishaji abiria bila
kuwa na leseni ambapo kati ya Desemba 12 mwaka jana hadi Mei 6 mwaka
huu, alitumia gari katika barabara ya umma aina ya Mitsubishi Rossa T.
871 BYS, kubeba wanafunzi.
Alidai shitaka la pili ni kuruhusu gari hilo kutumika bila kuwa na bima kati ya Desemba 16 mwaka jana na Mei 6 mwaka huu.
Shitaka
la tatu ni kushindwa kuingia mkataba na mwajiriwa wake kati ya Juni
Mosi mwaka jana hadi Mei 6, mwaka huu akiwa mmiliki wa gari hilo
alishindwa kuingia mkataba wa ajira kinyume na sheria za ajira na dereva
wake, Dismas Gasper ambaye kwa sasa ni marehemu.
Katika
shitaka la nne, Moshi anadaiwa kubeba na kuzidisha abiria 13 ambako
Mei 6, mwaka huu akiwa Mmiliki wa Kampuni ya Lucky Vincent, katika
maeneo ya Kwa Morombo, aliruhusu gari hilo kubeba abiria 38 badala ya
abiria 25.
Katika
kesi hiyo, Nkama anakabiliwa na shitaka moja ambalo ni kuzidisha abiria
katika chombo cha usafiri ambako akiwa mwandaaji wa safari hiyo ya
wanafunzi aliruhusu abiria zaidi ya 13 kupanda katika gari hilo ambalo
lilipaswa kuwa na abiria 25.
Baada
ya kusomewa maelezo hayo Moshi alikiri gari hilo kwenda Karatu likiwa
halina bima huku Mwalimu Mkuu Msaidizi akikiri kuwa alizidisha abiria
katika safari hiyo.
No comments:
Post a Comment