Tanzania
imeporomoka nafasi sita katika utafiti wa ukarimu duniani ikiwa ni
mwaka mmoja baada ya kufanya vizuri, jambo linaloonyesha Watanzania
wameanza kuwa na mkono wa birika katika kuchangia wenye uhitaji.
Ripoti
mpya ya ukarimu ya mwaka 2017 iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita
inabainisha sasa Tanzania inashika nafasi ya 63 duniani kutoka 57 mwaka
jana, nyuma ya majirani Kenya na Uganda katika ukanda wa Afrika
Mashariki.
Katika
ripoti hiyo ya kila mwaka inayoandaliwa na asasi ya kiraia ya kimataifa
kutoka Uingereza ya Charities Aid Foundation (CAF), inaonyesha Tanzania
imeanguka katika vipengele viwili kati ya vitatu ambavyo hutumika
kupima ukarimu wa watu wa nchi husika.
Mwaka
jana, Tanzania ilifanya vyema katika utafiti huo katika vipengele vyote
vya kumsaidia usiyemjua, kuchangia fedha na kujitolea muda kwa ajili ya
kuwasaidia wale wenye uhitaji.
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo ya nane, ni rahisi kwa Mtanzania kukupatia fedha
lakini si kupoteza muda wa kukusaidia au kukuhudumia iwapo hakufahamu.
Katika
ripoti ya mwaka huu, Tanzania inashika nafasi ya 110 katika kipengele
cha kujitolea muda kwa wenye uhitaji na nafasi ya 60 kati ya 138
zilizofanyiwa utafiti duniani katika kipengele cha kusaidia wageni
wasiofahamika.
Ni
kipengele kimoja tu cha kujitolea fedha ambacho Tanzania imepaa kwa
nafasi 13 kutoka nafasi ya 49 mwaka jana hadi nafasi ya 36 mwaka huu
ikiwa juu ya Uganda, Rwanda na Sudan Kusini.
Hii
ni kinyume cha Kenya ambao wanashikilia nafasi ya pili duniani katika
kipengele cha kujitolea muda kwa wenye uhitaji na nafasi ya nne kwa
kumsaidia mgeni wasiyemjua. Kenya ni nchi ya tatu duniani kwa ukarimu.
Hata
hivyo, ripoti ya utafiti huo uliofanywa mwaka jana inabainisha kuwa,
licha ya ukarimu kushuka kwa jumla duniani mwaka jana, bado Afrika
imefanya vyema baada ya wastani wa ukarimu kupanda kwa kila kipengele.
“Afrika
mwaka huu imeenda kinyume cha mwenendo wa dunia na ndiyo Bara pekee
lililoshuhudia kupanda kwa tabia ya kujitolea katika vipengele vyote
vitatu itakapolinganishwa na wastani wa ukarimu kwa miaka mitano,”
inaeleza ripoti hiyo.
Myanmar ndiyo nchi yenye ukarimu zaidi duniani kwa mwaka wa nne mfululizo ikifuatiwa na Indonesia na Kenya.
Utafiti
huo ulifinyika katika nchi 138. Baadhi ya watu walioteuliwa kuwa
sampuli waliulizwa ni mara ngapi huwasaidia watu wasiowajua, kuchangia
fedha na kujitolea muda wao kwa wasiojiweza ili kupima kiwango cha
ukarimu wao.
“Ili
kuongeza tabia ya kujitolea miongoni mwa watu duniani, Serikali zote
zinatakiwa kuhakikisha asasi za kiraia zinadhibitiwa kwa haki na kwa
uwazi, zirahisishe mazingira ya watu kujitolea na kutoa motisha pale
inapobidi,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti
inaeleza, “Serikali pia, zihamasishe uwepo wa asasi za kiraia kama
sauti huru za maisha ya watu na kuheshimu haki za taasisi
zinazojiendesha pasipo kupata faida kuzungumzia masuala ya msingi ya
kitaifa.”
No comments:
Post a Comment